Mwaka wa masomo wafungwa bila ripoti nchini Kongo
23 Julai 2025Mfumo wa elimu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) umeyumba vibaya, baada ya mwaka wa masomo wa 2025 kufikia tamati bila wanafunzi kupatiwa ripoti rasmi za masomo. Katika shule nyingi za umma, hususan mjini Kinshasa, wanafunzi waliondoka likizoni mikono mitupu – bila nyaraka muhimu zinazotumika kupandisha darasa au kuthibitisha maendeleo yao kitaaluma.
Katika mahojiano na DW, Christine Bijika, mzazi kutoka Kinshasa, alieleza hasira na kuchanganyikiwa kwake:
"Kama mzazi, hali hii inashtua sana. Nimejinyima kila kitu: kulipa ada, kuwapa watoto wangu moyo… Kisha wanarudi nyumbani bila ripoti. Huo ni ukosefu wa heshima kabisa. Ripoti si karatasi tu — ni ushahidi wa kazi ya mwaka mzima.”
Hali kama hiyo ilijirudia pia huko Bunia, katika jimbo la Ituri, ambako baadhi ya shule zilichukua hatua ya dharura kutengeneza ripoti zisizo rasmi. Ingawa hatua hiyo iliwasaidia wazazi kupata mrejesho fulani wa kitaaluma, ilizua maswali kuhusu uhalali wa nyaraka hizo.
David Mputu, mzazi kutoka Bunia, alisema: "Tulilipa faranga 1,000 kwa kila mwanafunzi. Serikali haikutuletea ripoti. Kila shule imetengeneza karatasi yake. Hizi si ripoti halali! Na mtoto akihitaji kuhamia shule nyingine? Atathibitisha vipi masomo yake?”
Goma: Ripoti kutoka kwa waasi badala ya serikali
Mashariki mwa Kongo, hali imechukua mkondo wa kisiasa. Katika mji wa Goma, unaodhibitiwa na waasi wa M23 AFC, ripoti za masomo zilitolewa—lakini si na serikali. Badala yake, waasi waliendesha zoezi hilo, wakiwataka wanafunzi kulipa faranga 1,000 ili kupata ripoti zilizotiwa saini.
Hali hiyo imezua hofu kubwa miongoni mwa wazazi. Mmoja wao ambaye hakutaka kutaja jina alisema:
"Hili halijawahi kutokea. Serikali kuu inaweza kukataa kutambua ripoti hizi baadaye. Hatujui nini kitatokea waasi wakiondoka. Ndiyo maana serikali inapaswa kuchukua jukumu lake.”
Mpaka sasa, serikali ya DRC haijatoa maelezo yoyote rasmi kuhusu kutokuwepo kwa ripoti za masomo au mpango wa dharura wa kuzitoa. Wanafunzi maelfu wamesalia njia panda – wakihofia kutopanda darasa au kushindwa kujiunga na taasisi nyingine kwa sababu ya ukosefu wa nyaraka za kitaaluma.
Kwa sasa, mfumo wa elimu nchini Kongo unakabiliwa na mtihani mkubwa wa uhalali, usimamizi na uaminifu – huku familia zikisalia na swali moja kuu: je, haki ya elimu ya watoto wao inaheshimiwa?