Wanadiplomasia wa Ujerumani, Marekani wakutana Washington
29 Mei 2025Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Johann Wadephul,ambaye aliteuliwa mapema mwezi huu baada ya Kansela Friedrich Merz kushika madaraka, yupo ziarani nchini Marekani kwa mazungumzo ya kidiplomasia yanayolenga kuimarisha uhusiano wa Berlin na Washington.
Wadephul alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, ambapo walijadili kwa kina mzozo wa Urusi na Ukraine. Katika mkutano wao wa dakika 45, wawili hao walisisitiza mshikamano wao dhidi ya uvamizi wa Moscow na kuonya kuwa vikwazo vipya viko mbioni iwapo Urusi itaendelea kukaidi juhudi za amani.
"Suluhisho la mazungumzo lazima lipatikane sasa. Na Urusi inatolewa wito kujiunga na mazungumzo… kila mtu anasubiri. Na daima imekuwa wazi kwamba barani Ulaya na hapa Marekani, kuna utayari wa kuchukua hatua endapo hili halitatimia.”
Waziri Wadephul alieleza kuwa Ujerumani iko tayari kushiriki kikamilifu katika juhudi za Marekani kusaidia Ukraine, ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa makombora ya masafa marefu yatakayomilikiwa moja kwa moja na Kyiv bila masharti kutoka kwa NATO. Hatua hiyo inatarajiwa kuwekewa msingi wa kisiasa katika mkutano ujao kati ya Kansela Merz na Rais Donald Trump.
Mazungumzo kuhusu mashariki ya kati na Iran
Katika kikao hicho, Wadephul pia alielezea wasiwasi kuhusu hali tete ya Mashariki ya Kati na kuongezeka kwa mvutano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. Alisisitiza kuwa mazungumzo ya kidiplomasia ni njia pekee ya kuzuia vita:
"Tunashirikiana na Marekani kutafuta suluhisho la mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran... pande zote zinazohusika zinatambua kuwa hii ndiyo njia bora ya kutatua mzozo huu.”
Wadephul aliitaka Israel kuwa na tahadhari kuhusu hatua za kijeshi dhidi ya miundombinu ya nyuklia ya Iran, akisisitiza kuwa njia ya kidiplomasia ni salama zaidi kwa kanda hiyo nzima.
Shughuli nyingine na ujumbe wa kidiplomasia
Waziri huyo alitumia muda wake mjini Washington kuwapa heshima waathirika wa shambulizi la karibuni dhidi ya wafanyakazi wa ubalozi wa Israel kwa kuweka maua katika Jumba la Makumbusho la Wayahudi. Aidha, alikutana na Katibu Mkuu wa Shirika la Nchi za Amerika (OAS), Albert Ramdin, ambapo walijadili masuala ya demokrasia, uhuru wa vyombo vya habari na amani ya kimataifa.
Ingawa hakufanikiwa kukutana na baadhi ya viongozi mashuhuri wa Marekani kama kawaida ya ziara za kwanza za kidiplomasia, Wadephul alifanya mazungumzo na viongozi wa taasisi za utafiti na kuendeleza uhusiano na Rubio, mshirika wa karibu wa Rais Trump.
Kwa heshima ya siku ya kuzaliwa ya Rubio, Wadephul alimzawadia bango la timu ya mpira wa miguu ya Miami Dolphins, ishara ya uhusiano wa karibu wa kidiplomasia unaoendelea kujengeka kati ya Marekani na Ujerumani.