Wanadiplomasia wa magharibi wahimiza utawala bora Pakistan.
10 Mei 2023Katika mkutano waó wa pamoja wa waandishi wa habari mjini Washington, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje Antony Blinken alisema wanataka kuhakikisha kwamba chochote kitakachotokea Pakistan kinaendana na utawala wa sheria, na katiba. Akizungumza akiwa pembeni mwa Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza James Cleverly, alibainisha kuwa taifa lake linafurahishwa na uhusiano wa muda mrefu na wa karibu na mwanachama wa Jumuiya ya Madola Pakistan. Hata hivyo wote wawili walikataa kutoa maoni yao kwa undani zaidi kuhusu kukamatwa kwa Imran Khan, huku Cleverly akisema kuwa hajafahamishwa kikamilifu kuhusu mkasa huo. Khan, ambaye aliondolewa madarakani mwaka jana kama waziri mkuu wa kiraia wa taifa hilo la tano kwa idadi kubwa ya watu duniani, alikamatwa wakati alipofika mahakamani Jana Jumanne mjini Islamabad kutokana na moja kati ya kesi nyingi zinazomkabili.