Israel na Palestina zaalikwa Brussels
14 Julai 2025Wanadiplomasia wa ngazi za juu kutoka Israel na mamlaka ya Wapalestina wanashiriki hivi leo mjini Brussels mkutano kati ya Umoja wa Ulaya na majirani zake wa upande wa Kusini.
Waziri wa mambo ya nje wa Israel,Gideon Saar anatarajiwa kufanya mazungumzo na mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas pamoja na kamishna wa Umoja huo anayehusika na nchi za kanda ya bahari ya Meditterania Dubravka Suica.
Mamlaka ya Wapalestina mjiniRamallah, imethibitisha kwamba waziri wake wa mambo ya nje Varsen Aghabekian Shahin atashiriki mkutano huo ingawa imekanusha ripoti kwamba mwanadiplomasia wake huyo atakutana na Gideon Saar.
Mkutano huo wa Brussels utajadili kuhusu hali ya Ukingo wa Magharibi ambako vurugu zinaongezeka na Israel imekuwa ikiendeleza operesheni ya kijeshi Kaskazini wa eneo hilo na kuwaacha bila makaazi maelfu ya Wapalestina.