Walimu wa maeneo ya M23 wanyimwa mishahara kwa miezi sita
24 Juni 2025Hatua ya kugoma inafuatia mazungumzo ya Juni 10 mwaka huu, ambapo walimu walituma wawakilishi Goma kuzungumza na maafisa wa serikali kuhusu malimbikizo ya mishahara, bila mafanikio.
Felix Hakiza, Katibu Mkuu wa Muungano wa Kitaifa wa Walimu wa Shule za Umma huko Rutshuru, anasema kuna maeneo ambayo migomo inaendelea, na kwa miezi kadhaa wanafunzi hawajasoma isipokuwa wa darasa la sita wanaojiandaa na mitihani ya kumaliza elimu ya msingi.
"Baadhi ya shule hazijaanza masomo tangu Machi. Kuna walioacha shule, wengine wameolewa mapema na baadhi ya watoto wamejiunga na makundi ya waasi. Hii inaharibu kabisa elimu yetu” alisema Hakiza.
Wazazi walalamikia hali ya kielimu
Mmoja ya wazazi Jean Harerimana anaeleza kwa masikitiko kwamba "Watoto wangu hawajaenda shule kwa karibu miezi minne. Baadhi ya shule zilifungwa Februari kwa sababu walimu hawakulipwa. Kwa kuwa elimu ni bure, serikali inapaswa kuwalipa walimu. Athari zake ni mbaya sana.”
Chama cha Walimu kinasema walimu katika maeneo hayo hawalipwi mishahara. Shirika la misaada la Caritas ambalo awali lilikuwa lilikuwa likiwalipa haliwezi tena kufanya hivyo tangu uasi wa M23.
M23 wadai serikali inatumia fedha za walimu
Kwa upande wao muungano wa kisiasa na kijeshi wa M23 umesema walimu wa Rutshuru, Masisi na Nyiragongo ni sehemu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hivyo wanapaswa kulipwa kama walimu wengine nchini humo.
Wameshutumu serikali kwa kufunga akaunti za benki za walimu hao, wakidai hiyo ni adhabu kwa wakaazi wa maeneo hayo.
Kundi hilo pia limedai kuwa serikali ya Kinshasa inatumia fedha za walimu hao vibaya na sasa wameanza mashauriano na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF kutafuta suluhu kwenye maeneo wanayoyadhibiti.
Hadi sasa, serikali ya Kinshasa haijatoa tamko lolote kuhusu madai hayo na walimu wakijishughulisha na mambo mengine nje ya taaluma yao.