Umoja wa Ulaya kujadili Ukraine, ulinzi na uchumi
26 Juni 2025Viongozi hao wanatazamiwa kuzungumza kuhusu kurefusha vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi na kuchukua hatua nyingine dhidi ya taifa hilo.
Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban hata hivyo tayari amelizungumzia suala jingine linaloweza kupewa nafasi kwenye mkutano huo zikiwemo juhudi za Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya. Amesema, kama Ukraine ikiingizwa kwenye Umoja wa Ulaya jumuiya hiyo itakuwa imejitumbukiza vitani. Amefafanua kuwa sababu ni kwamba kama nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya ikiwa vitani, basi Umoja wa Ulaya utakuwa moja kwa moja vitani na hilo halipaswi kutokea.
Soma zaidi: Umoja wa Ulaya kurejesha upya vikwazo dhidi ya Urusi
Kwa upande wake Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Antonio Costa amesisitiza kuwa Umoja wa Ulaya utaendelea kuiunga mkono Ukraine. Ulinzi, na uchumi wa Ulaya vinatazamiwa kuwa sehemu ya ajenda za mkutano huo, huku Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz akisema mzozo wa kibiashara kati ya Umoja na Marekani hauna budi kutatuliwa mara moja.