Wakuu wa EAC/SADC waumulika mzozo wa Kongo
8 Februari 2025Akifungua mazungumzo hayo, Ruto amesema majadiliano hayo ni jitihada zinazofanywa na jumuiya mbili kwa kukutana kwa pamoja katika kutafuta suluhu ya mgogoro wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa njia zinazozingatia misingi ya kidemokrasia.
"Kukubaliana kwetu ni sawa na kuchukua hatua na pia kuwaonea huruma mamilioni ya watu ambao wapo katika hatari ya kupoteza maisha na maendeleo ya kiuchumi."
Rais wa Kenya William Samoei Ruto, amesema mazungumzo ya amani sio udhaifu bali ni busara ya pamoja na yanaonyesha usikivu wenye lengo la pamoja la kupata matokeo mazuri badala ya vita.
Mwenyekiti wa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Emmerson Mnangagwa, amesema mkutano huuni ushahidi wa dhamira ya jumuiya za EAC/SADC kwamba juhudi zinaweza kuwezesha kuchukuliwa hatua za haraka ili kusitisha vita nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mnangagwa amesema:
"Hali tete inayoendelea na migogoro iliyoponchini Kongo, inasababisha madhara makubwa sio kwa Kongo tu bali hata katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika,(SADC)."
Rais Mnangagwa ameongeza kusema kuwa Afrika inatakiwa kushikamana kama ilivyoshikamana wakati wa kutafuta uhuru kutoka kwa wakoloni. Amesema:
"Tutumie fursa hii, kuwa na suluhisho la pamoja ambalo lina lengo la kukomesha vita na kuleta amani ya kudumu."
Kwa upande wake, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania itaendelea kusaidia mipango yote ya kidemokrasia ili kukomesha mapigano nchini Kongo.
"Ombi langu kwenu, tutafute jitihada za kukomesja machafuko DRC na kuleta amani."
Rais Samia amesema viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, (SADC) hawawezi kukaa kimya wakati nchi hizo zina wajibu wa kuushughulikia mgogoro wa mashariki mwa Kongo.