Wakuu wa majeshi Afrika wakutana kujadili usalama na amani
28 Mei 2025Kongamano hilo linafanyika barani Afrika kwa mara ya pili na kuwaleta pamoja wakuu wa usalama kutoka mataifa 37. Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi, kamanda Jenerali wa kikosi cha Marekani barani Afrika cha AFRICOM, Michael Langley ameusisitizia umuhimu wa kuimarisha ushirikiano ili kukabiliana na vitisho vinavyoibuka barani Afrika ili kudumisha usalama na ustawi.
Kwa upande wake waziri wa ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, alilihutubia kongamano kielektroniki siku ya Jumatatu kuusisitizia umuhimu wa ushirikiano wa Marekani na Afrika ili kupambana na changamoto za kiusalama zinazoibuka. Kauli hizo zinaungwa mkono na waziri wa ulinzi wa Kenya, Soipan Tuya.
"Kenya na Marekani ina ushirikiano thabiti wa ulinzi.Kongamano hili linatupatia jukwaa muhimu la majadiliano yaliyo na msingi wa ajenda ya Afrika na kutambua kuwa amani endelevu inapatikana kwa ushirikiano wa kikanda na kimataifa."
Ushirikiano, ubia na muingiliano wa mikakati
Mada kuu ya mkutano huo wa usalama ni Kuimarisa usalama Afrika, kudumisha ustawi wa juhudi za pamoja. ACHOD25 imekuwa jukwaa muhimu la majadiliano rasmi na kubadilishana mitazamo katika sekta ya usalama. Rais William Ruto alibainisha kuwa usalama ni ajenda ya kila taifa na mifumo inategemeana.
"Usalama unavuka mipaka ya nchi yoyote ile…ushirikiano, ubia na muingiliano ndiyo njia mwafaka za kuwa na usalama na ustawi nje na ndani ya mataifa yetu", alisema Ruto.
Kongamano la mwaka uliopita lilifanyika mjini Gaberone nchini Botswana. Mwaka huu, mkutano huo unafanyika chini ya ulinzi mkali hapa jijini Nairobi.
"Kimsingi vikao hivi ni vya kuwatuliza wadau wa kimataifa"
Je, vikao vya aina hii vina mchango upi katika kudumisha usalama wa mataifa ya Afrika? Hilo ndilo suali nililomuuliza John Musundi, mchambuzi wa masuala ya usalama.
"Marekani ina wasiwasi na hofu kuwa ushawishi wake utapungua barani Afrika ukizingatia kuwa baadhi ya mataifa ya Afrika hasa yaliyo na utajiri wa madini yanageukia utawala wa kijeshi. Kimsingi vikao hivi ni vya kuwatuliza wadau wa kimataifa", alielezea Musundi.
Kongamano hilo linaungwa mkono na washirika wa kimataifa ila ajenda inaongozwa na vipaumbele vya mataifa ya Afrika.