Wakulima wa parachichi Kenya wanufaika na uvumbuzi mpya
14 Mei 2025Mashamba ya maparachichi yaliyoko Meru yamenawiri na kustawi.Miti ya parachichi imesheheni kwenye mashamba yaliyo chini ya Mlima Kenya ambako hewa ni safi, maji ni mengi na matunda yananing'inia yakisubiri kukomaa.
Kilimo cha parachichi sasa ni cha kutegemewa.Kenya ndiye muuzaji mkubwa wa maparachichi barani Afrika na moja ya mataifa kumi bora kote duniani.Kulingana na takwimu za idara rasmi, KNBS, Kenya ilijikusanyia pato la shilingi bilioni 19 mwaka 2023 na kiwango hicho kinatabiriwa kuongezeka hasa baada ya marufuku ya muda ya kuuza matunda hayo kuondolewa mwishoni mwa mwaka 2024.
Taa malum inawafukuza nondo usiku
Hata hivyo kipo kitisho kilichojificha kinachovamia matunda. Kifaa kinachotumia miale ya jua ndiyo suluhu kwa wadudu wanaovamia maparachichi. Taa ya sola inawaka wakati wa usiku baada ya kupokea miale ya jua mchana kutwa. Nondo huvamia maparachichi wakati wa usiku na kuyaacha yakiwa na mashimo.
Mwangaza huwavutia nondo ambao wanadondoka kwenye beseni la maji ya sabuni kama anavyoelezea Mutuma Muriuki muasisi wa Eco Bristo inayotengeza mashine hii, "Hiki kifaa kinasaidia kumaliza wadudu wa shamba bila kuwaathiri wale wa manufaa kama vile nyuki na vipepeo ambao ni wadudu wa mchana. Hiki kifaa kinamaliza wadudu wakati wa usiku.Usiku kuna aina maalum ya nondo, FCM, ambao hutoboa matunda na kuyaacha na weupeweupe.Hilo beseni ni la kuwatega hao waudud,Wakipepea karibu na taa, wanadondoka na kunasa kwenye maji ya sabuni."
Mutuma Muriuki ni mshindi wa tuzo maalum za kuunga mkono teknolojia na uvumbuzi kwenye kilimo za mpango wa AYuTe wa shirika la maendeleo ya kilimo la Heifer International. AyuTe Africa Nextgen ilizinduliwa 2021 kama njia moja ya kukuuza vipaji vya vijana kuzindua suluhu za kiteknolojia zinazodhamiria kuwapa afueni wafanyabishara wadogo wa kilimo.
Agnes Kavatha ni meneja wa uvumbuzi na vijana katika shirika la Heifer International na anasisitiza kuwa hatima ya kilimo iko mikononi mwa vijana na,"Kama mradi, huwa tukianza tunawapiga jeki.Pale mradi unapokwisha, hao vija huwa wameshikana na wakulima lakini hatuwezi kuendelea kuwapa kiinua mgongo.Hiyo ndiyo sababu ya kuwashirikisha wadau wa sekta ya binafsi ili wafanye kazi pamoja na wakulima kuwafikishia huduma wanazohitaji kwa kutumia teknolojia huko mashinani ndipo wapate malipo kupitia sekta hiyo."
Ushindani kwenye soko la kimataifa
Heifer International inayofadhili miradi ya kilimo na maendeleo ilizindua mkakati wa miaka mitano unaolenga kuimarisha biashara za wakulima wadogo na miradi ya kuhimili madhara ya mabadiliko ya tabianchi.Mkakati huo mpya PC4 unawalenga zaidi wanawake na vijana kutumia teknolojia na mbinu za kisasa za kilimo na ufugaji wa wanyama.
Maparachichi ya Kenya aghalabu huuzwa Ulaya inayoweka vigezo vikali vya usalama mintarafu utumiaji wa madawa.Uholanzi ndiyo inayonunua kiasi ya nusu ya maparachichi yanayopandwa Kenya.
Hata hivyo matunda ya Peru, Mexico na Afrika Kusini yanaipa Kenya ushindani mkubwa kwenye soko la kimataifa. Kwa upande wake, serikali ya Kenya ilitangaza hatua ya kulifungua tena soko la kuuza nje maparachichi baada ya kipindi cha miezi kadhaa ya kukagua miti, mazao na mikakati.
Shehena ya maparachichi hususan aina za Hass, Fuerte na Pinkerton zilisitishwa kusafirishwa mwishoni mwa Oktoba 2024 kwa kuhofia ubora wa matunda hayo ambayo ilisadikika hayakuwa yamekomaa.
Vita dhidi ya nondo vyaimarika bila kemikali
Wakulima wa wadi ya Abogeta West wamegeukia matumizi ya kifaa cha kunasa nondo ili kuokoa zao lao la parachichi. Kinyua Nkanata ni mwenyekiti wa chama cha wakulima wa parachichi huko Abogeta West na anausifia uzinduzi huu kwani, "Wakulima wetu wanachama wamegeukia matumizi ya teknolojia hiyo ya kifaa cha kunasa nondo kinachotumia miale ya jua. Tayari zaidi ya wakulima 50 wanaitumia teknolojia hii. Ijapokuwa ni uvumbuzi mpya bado wengine wengi wanaendelea kuifahamu na kuipokea."
Nondo wamekuwa wakiwatatiza wakulima wa parachichi ambao baadhi walipoteza tani nyingi za zao hilo. Uzinduzi huu umewaweka wakulima wa parachichi katika nafasi nzuri sokoni hasa Ulaya.
Uamuzi wa Kenya wa kubana zaidi na kuweka vigezo vikali vya kuuza nje maparachichi unajumuisha pia matunda yanayotokea mataifa jirani ya kanda nzima ya Afrika Mashariki, EAC.
Maparachichi yanayoingia Kenya kwa minajili ya kuuzwa nje ya mipaka yake sharti yaandamane na hati mwafaka na yatimize vigezo vilivyowekwa vya ukaguzi ukizingatia matumizi ya dawa na kemikali na njia za usafirishaji.