Wakristo kote duniani wamuombea Papa Francis
23 Aprili 2025Kuanzia Vatican, Roma na maeneo mbalimbali barani Ulaya, Afrika, Amerika ya Kusini, Jerusalem, Asia na kwengineko, wakristo wanaendelea kuomboleza na kufanya ibada ya kumuombea Papa Francis . Misa takatifu imefanyika leo Jumatano katika Kanisa la Kaburi Takatifu huko Jerusalem.
Baadhi ya waumini wameonekana wakilia huku wengine wakiwasha mishumaa na kupiga magoti kwenye Jiwe la Upako huko Jerusalem ambapo kulingana na imani ya Kikristo, inaaminika kuwa mwili wa Yesu Kristo uliandaliwa kwa mazishi.
Mjini Vatican, maelfu ya watu wameanza kuuaga na kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Papa Francis ambaye leo hii ulipelekwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro. Manu Kasten anayeishi Guadalajara ni mmoja wao aliyeelezea hisia zake wakati akiongoza kundi la mahujaji kutoka Mexico:
"Mwanzoni tulijawa na huzuni na hisia mseto ikiwa ni pamoja na furaha, hali ya utulivu na kumbukumbu nyingi. Hakika kuna wakati moyo ulihuzunika tulipobaini kuwa ndiyo mara ya mwisho tunamuona hadharani, lakini tukiwa na matumaini ya kufahamu kwamba sasa yuko mahali anapostahili."
Harakati za mazishi na kumchagua Papa Mpya
Papa Francis aliyechaguliwa kuliongoza Kanisa hilo mwaka 2013, atazikwa Jumamosi hii katika Kanisa alilolipenda zaidi la Mtakatifu Maria Maggiore mjini Roma, mazishi yanayotarajiwa kuhudhuriwa na viongozi kutoka mataifa mbalimbali duniani. Nchi kama Italia, Slovakia, Ufilipino na nyingine zimetangaza siku tofauti za maombolezo hadi Papa atakapozikwa siku ya Jumamosi.
Soma pia: Mwili wa Papa Francis wawasili Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro
Kufuatia kifo cha Papa Francis mwenye umri wa miaka 88 ambaye jina lake halisi ni Jorge Mario Bergoglio raia wa Argentina, mchakato wa karne nyingi wa kumchagua Kiongozi Mpya wa Kanisa Katoliki Duniani unaohusisha ibada, viapo vitakatifu, mkusanyiko wa makadinali wanaopiga kura na kadhalika vitaanza mara moja baada ya mazishi ya siku ya Jumamosi.
Baada ya kura hiyo inayofanyika kwa siri, moshi mweupe huashiria kuwa Makadinali wamemchagua kiongozi mpya wa Wakatoliki bilioni 1.3 kote duniani, na moshi mweusi ni ishara kwamba makadinali hao hawajafikia maamuzi na kwamba mchakato huo utaendelea. Wakati wa zoezi hilo makadinali wanaopiga kura ya kumchagua Papa mpya hawaruhusiwi kuwa na mawasiliano yoyote na watu walio nje ya chumba hicho.
(Vyanzo: Mashirika)