Wakimbizi 6,000 wakimbia kambi Kenya kwa uhaba wa misaada
29 Agosti 2025Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limeripoti kuwa zaidi ya wakimbizi 6,200 kutoka Sudan Kusini wameondoka katika kambi ya Kakuma na makaazi ya jirani ya Kalobeyei, kaskazini mwa Kenya, tangu mwezi Januari mwaka huu.
Kati ya Julai hadi Agosti 22 pekee, takriban wakimbizi 3,600 wengi wao wakiwa wanawake na watoto waliondoka katika kambi hiyo kupitia njia rasmi na zisizo rasmi.
Kambi ya Kakuma, ambayo ni ya pili kwa ukubwa nchini Kenya, inahifadhi takriban wakimbizi 300,000 kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Sudan Kusini, Somalia, Uganda na Burundi. Hata hivyo, mashirika ya kibinadamu yanakabiliwa na ukata mkubwa wa fedha, hali iliyosababisha maandamano na ghasia mwezi uliopita baada ya kupunguzwa kwa mgao wa chakula.
Tangu mwezi Julai, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeanza kupunguza mgao wa chakula kwa wakimbizi, likielekeza misaada katika maeneo yenye uhitaji mkubwa zaidi. Hatua hiyo imewaacha baadhi ya wakimbizi bila msaada wa chakula, na kusababisha ongezeko la idadi ya wakimbizi hao kuondoka.
Baadhi ya wakimbizi warudi makwao
Afisa wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi (DRS) aliyepo Kakuma aliyekataa kutajwa jina lake ameeleza kuwa wakimbizi wengi wanaondoka kwa sababu hawapati tena msaada wa chakula. Wengi wao wanarudi Sudan Kusini, licha ya mazingira ya hatari yanayoendelea nchini humo.
Sudan Kusini imekuwa ikikumbwa na machafuko kwa miaka kadhaa, na kwa sasa inakabiliwa na hatari ya kuzuka kwa vita vipya vya wenyewe kwa wenyewe. Hali hiyo imeendelea kuwasukuma raia wake kutafuta hifadhi nje ya mipaka ya nchi hiyo.
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani limeonya kuwa bila rasilimali zaidi kupatikana haraka, wakimbizi wengi watalazimika kuchagua kati ya kuishi na njaa kambini au kurejea katika mazingira ya hatari.
UNHCR imeeleza pia kuwa ingawa uhamaji wa wakimbizi si jambo jipya, ila idadi ya wanaondoka katika kambi hio wengi na jambo ambalo litasababish shirika hilo kuendelea kufuatilia hali hio kwa karibu.