Wakimbizi wa Msumbiji nchini Malawi kurejea nyumbani
9 Julai 2025Katika uchaguzi huo Daniel Chapo wa chama tawala cha Frelimo alichukua nafasi ya Rais Filipe Nyusi aliyemaliza muda wake kikatiba, huku kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane akidai kuwa uchaguzi uligubikwa na udanganyifu, hatua iliyosababisha maandamano makubwa katika taifa hilo la kusini mwa Afrika.
Mahakama ya Katiba ya Msubiji ilithibitisha ushindi wa Chapo na kuhakikisha utawala wa muda mrefu wa chama cha Frelimo tangu taifa hilo lilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Ureno mnamo mwaka 1975.
Wanasiasa wa upinzani walizidi kuweka shinikizo kwa mamlaka juu ya udanganyifu katika zoezi la uchaguzi huku vikosi vya usalama vikikabiliana vilivyo na waandamanaji katika miji muhimu ikiwemo Maputo.
Kufuatia machafuko hayo ya baada ya uchaguzi idadi kubwa wa watu walikimbilia katika eneo la Nsanje kusini mwa taifa jirani la Malawi huku wakikabiliana na changamoto kadhaa wakiwa njiani kunusuru maisha yao.
Hali ya wakimbizi hao nchini Malawi ni tete. Malawi, moja ya nchi maskini zaidi duniani kulingana na Benki ya Dunia, tayari inawahifadhi wakimbizi zaidi ya 50,000.
Soma pia:Raia waripotiwa kuuawa katika mashambulizi mapya kaskazini mwa Msumbiji
Kutokana na ongezeko la wakimbizi wa Msumbiji limeongeza mzigo kwa nchi hiyo ambayo inakabiliwa na ukame na uhaba wa chakula kutokana na athari za El Niño.
Mwanaharakati wa haki za binadamu na Mkurugenzi wa shirika la Nyika, Moses Mukandawire ameiambia DW kwamba Malawi inayo uzoefu wa kushughulikia mzozo wa wakimbizi wa Msumbiji akirejelea wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1977 hadi 1992.
"Ni changamoto na ukizingatia hatuna uhakika wa asilimia moja kwamba amani imerejea Msumbiji."
Aliongeza kwamba "machafuko ya baada ya uchaguzi yaliowasababisha wao kukimbia inasikitisha kwamba wengi walipoteza mali zao, wengi walikimbia makaazi yao ndio maana tukawa na wakimbizi wengi."
Aidha alitoa wito wa usalama miongoni mwa wakimbizi hao ikiwemo hakikisho la kutokuwepo kwa vitisho miongoni mwao.
Lakini kwa wengi uhakika huo haupo, kutokana na ukweli kwamba hakuna kilichosalia katika mali na jamaa zao hasa baada ya ghasia hizo za uchaguzi. Mbali na madhara ya kibinadamu, ghasia hizi zimekuwa pigo kubwa kwa uchumi wa Msumbiji.
Athari za kiuchumi zinashuhudiwa pia
Chama cha wafanyabiashara kinasema kuwa biashara zaidi ya 1,000 zilifungwa kutokana na uporaji na uharibifu huku asilimia 40 ya miundombinu ya biashara ikiharibiwa.
Inakadiriwa hasara ya kiasi cha yuro milioni 110 kwenye hisa na miundombinu huku takriban watu 17,000 wakipoteza ajira.
Serikali ya msumbiji pia imeripoti zaidi ya yuro milioni 600 kupotea kwenye mapato yanayotokatana na kodi kufuatia machafuko hayo.
Soma pia:Chapo aahidi kuiunganisha Msumbiji
Mtaalamu wa masuala ya uchumi Teresa Boene anasema kuwa, kwa sasa linalotakiwa kupewa kipaumbele ni kurejesha utulivu wa kiuchumi na kuunda mazingira bora ya biashara.
Kuimarika kwa hali katika taifa hilo la kusini mwa Afrika kunategemea na namna ambavyo serikali itakavyoshughulikia malalamiko ya upinzani, kuimarisha hali ya uchumi na mdororo wake na kurejesha imani ya wananchi wake.