Wakimbia, wajeruhiwa, na kusahaulika msitu wa mpakani Poland
6 Julai 2025Aleksandra Chrzanowska anasimama kwa muda, anakagua mahali alipo kupitia simu yake ya mkononi, kisha anaingia moja kwa moja msituni bila kufuata njia yoyote. Anatembea kwa kujiamini, licha ya ardhi ya tope na isiyo sawa.
Hifadhi ya Taifa ya Bialowieza ni msitu wa mwisho wa asili uliohifadhiwa barani Ulaya. Tangu mwaka 2021, Chrzanowska, ambaye ni mwanachama wa shirika la haki za binadamu lenye makao makuu Warsaw linaloitwa Association for Legal Intervention, amekuwa akitembelea msitu huo karibu kila siku.
Hii ilikuwa ni baada ya Belarus kuanza kuhimiza watu kutoka nchi za tatu kuvuka kuingia Poland kama njia ya kuiandama EU. Poland ilijibu kwa kujenga uzio mkubwa wa mpaka na kuwarudisha watu Belarus. Tangu wakati huo, hali kwenye mpaka huo imekuwa janga la kibinadamu.
Chrzanowska anaonesha ramani kwenye simu yake. Imejaa alama za rangi mbalimbali. Kila moja inawakilisha "ingilio la msaada wa kibinadamu,” kama wanaharakati wa mtandao wa Grupa Granica wanavyoita shughuli zao za kutoa msaada msituni kando ya mpaka wa Belarus.
Kawaida, hii inahusisha kuwapelekea wakimbizi supu ya moto, maji, nguo, viatu na betri za simu. Mara nyingi pia wanatoa msaada wa matibabu, wakisaidiwa na daktari iwapo hali ni mbaya.
Uzio wa chuma wa mita tano hausimamishi uhamiaji
Tangu uzio wa urefu wa mita tano kujengwa mpakani na Belarus, majeraha kama kuvunjika mifupa na kukatwa vibaya na waya wa chuma yameongezeka kwa kasi. "Uzio huo hauwezi kuwazuia watu,” asema Chrzanowska. "Hawana chaguo. Maisha yao yako hatarini katika nchi zao.”
Mwaka jana, Grupa Granica ilipokea simu za dharura takriban 5,600. Iliweza kuingilia kati katika matukio 1,400 na kuwasaidia watu 3,400. Wakimbizi hao walitokea Syria, Eritrea, Sudan, Somalia, na Afghanistan.
Katika mwaka huohuo, polisi wa mpaka wa Poland walirekodi takriban majaribio 30,000 ya kuvuka mpaka kinyume cha sheria. Idadi hiyo inaendelea kuongezeka: Frontex iliripoti kuwa mwaka 2024, idadi ya watu waliotumia njia ya mashariki kupitia Belarus iliongezeka kwa karibu asilimia 200.
Leo, Aleksandra Chrzanowska anaelekea eneo lililopangwa kuchukua vitu vilivyoachwa baada ya msaada uliopita. Grupa Granica huweza kutumia tena baadhi ya vitu hivyo, lakini muhimu zaidi, hawataki kuacha takataka katika hifadhi hii ya kipekee ya asili. Chrzanowska anavaa glavu za plastiki, anakusanya chupa ya thermos, koti lililoraruliwa, na kiatu cha mtoto, na kuvihifadhi kwenye mfuko wa taka.
Simu yake inapigwa. Kambi kuu inampigia. Mawasiliano si mazuri: Chrzanowska anatukana kwa hasira, lakini ameielewa ujumbe. Wanaume wawili wa Kiafghan wametuma ujumbe mfupi kwa nambari ya dharura ya kimataifa, wakiomba msaada.
"Tunahitaji kuharakisha,” asema. Ghafla, anabadilika kabisa. Anabeba mfuko wa taka, na tunapoanza kuelekea kambini, anasikiliza ujumbe wa sauti unaotoa maelezo ya msaada unaofuata.
Wamejificha ndani ya msitu
Mmoja wa wanaume hao ana majeraha makubwa, kwa mujibu wa ujumbe. Wakimbizi hao wa Kiafghan pia waliomba nguo kavu na viatu kwa sababu wamebaki na mavazi yaliyolowa kabisa. Wametuma picha ya jeraha, ambalo litatumwa kwa daktari kwa ajili ya ushauri. Wakati huo huo, kambini, wahisani wengine wanapakia vifaa wanavyohitaji wanaume hao katika mabegi makubwa.
Muda mfupi baadaye, Chrzanowska na mwanaharakati mwingine wanaanza kutembea kupitia njia ya msituni, kabla ya kuchupa kuingia ndani zaidi kwa sababu za kiusalama. Wanakutana na wakimbizi kwenye eneo walilolituma. Chrzanowska anasema wanaume hao walikuwa wamejificha vizuri; iliwachukua muda kuwapata.
Wanaume hao, walioko katika miaka yao ya ishirini, hawazungumzi Kiingereza. Wanaharakati wanatumia programu za kutafsiri kwenye simu, wakiandika maswali ambayo yanatafsiriwa kwa lugha ya Kipushtu. "Mmekaa muda gani msituni?” Wanaume wanaandika: wiki chache, siku tatu upande wa Poland. Ni jaribio lao la tatu; walirudishwa mara mbili kabla.
Hii inamaanisha walishakamatwa mara mbili na walinzi wa mpaka wa Poland na kurudishwa Belarus, licha ya kuwa wanatafuta hifadhi. Mnamo Machi 27 mwaka huu, Poland ilisitisha rasmi haki ya kuomba hifadhi kwenye mpaka wa Belarus.
Wanaume hao hawajakula wala kunywa kwa siku kadhaa. Wanakubali kwa shukrani supu ya dengu, chai tamu na maji waliyoletewa. Wanapopata nguvu kidogo, Chrzanowska anawasiliana kwa maandishi na daktari. Jeraha mguuni ni kubwa zaidi kuliko lilivyoonekana kwenye picha. Daktari anamtumia maelekezo ya jinsi ya kusafisha na kutibu jeraha hilo.
Mmoja anaandika kuwa alijeruhiwa alipoamrishwa kuruka kutoka kwenye uzio wa mpaka. Walikuwa wamesindikizwa na wanajeshi wa Belarus waliokuwa na silaha, waliowapiga.
Wanajeshi hao waliuweka ngazi kwenye uzio wa chuma wa mita tano, na kuwalazimisha Waafghan kuruka upande wa pili. "Kwa kawaida, tungeita gari la wagonjwa kutibu jeraha hilo ipasavyo,” asema Chrzanowska.
"Lakini tangu kusitishwa kwa utaratibu wa kuomba hifadhi, hilo ni hatari sana kwa sababu walinzi wa mpaka pia huwasili. Hilo humaanisha kuna hatari kubwa ya wakimbizi kurudishwa Belarus, hata kama wamejeruhiwa vibaya.”
Mashirika ya kusaidia ya ndani yameachwa peke yake
Muda wa msaada huo ni kama nusu saa. Chrzanowska anajaribu kusafisha jeraha kwa kadiri awezavyo. Anaporudi kambini, anaripoti kuwa yule mwanaume alikuwa amelala chini ya sakafu ya msitu, dhaifu sana na mwenye maumivu makali. "Nilihofia kuwa asingeweza kutembea tena,” asema. Lakini baada ya kula na kunywa, hali yake ilistahimilika.
Kwa Chrzanowska, huu ni wakati unaogusa moyo kila wakati. "Mara ya kwanza, wakimbizi huwa na hofu kubwa. Lakini baada ya kupata nguo kavu na supu ya moto au chai, unaona wanarejea kuwa binadamu tena.” Wengine huamua hata kugawana chakula na yeye.
Mtandao wa Grupa Granica unajumuisha mashirika kadhaa ya misaada ya kijamii na asasi za kiraia, ukisaidiwa na mamia ya wahisani pamoja na wachache wanaolipwa. Mbali na Madaktari Wasio na Mipaka, hakuna shirika lolote la kimataifa linalofanya kazi mpakani mwa Poland na Belarus — tofauti na mipaka mingine ya nje ya EU.
Serikali ya Poland inapinga kazi ya wanaharakati hawa, na inatuhumu utoaji wa msaada kwa wahamiaji kuwa ni kosa la jinai. Kwa sasa, wanaharakati watano wanashtakiwa katika mji wa mashariki wa Hajnowka kwa kuwasaidia familia ya Wakurdi wa Iraq wenye watoto saba waliokuwa wakijificha msituni. Wanashtakiwa kwa "kusaidia ukaaji wa wahamiaji haramu kwa faida binafsi.”
Lakini Aleksandra Chrzanowska hashtushwi. "Kuwasaidia watu si kosa la kisheria,” asema kwa mkato. Saa chache baadaye, wanapokea simu nyingine ya dharura.
Kundi la Waafghan wanne linaomba msaada. Mmoja anaripoti kuwa amevunjika mguu baada ya kuruka kutoka kwenye uzio wa mpaka. Safari hii, daktari ataambatana nao.