Wakfu wa hisani wa Trump hatimae wakubali kujivunja
19 Desemba 2018Mwanasheria mkuu wa jimbo la New York Barbara Underwood amesea Wakfu wa Trump umekubali kujivunja wenyewe chini ya usimamizi wa mamlaka za kisheria za nchini Marekani. Wakfu huo wa misaada wa Trump umedaiwa, wakati wote kuhusika na vitendo vilivyokwenda kinyume cha sheria. Mwanasheria mkuu huyo ameeleza kuwa rais Trump alikuwa analitumia shirika hilo la hisani kama kitabu chake cha hundi kwa ajili ya maslahi yake ya kibiashara na kisiasa.
Kwa mujibu wa wakili huyo wa jimbo la New York wakfu wa Trump ulionyesha mfumo wa kwenda kinyume cha sheria, ikiwa pamoja na kuratibisha kampeni ya Trump wakati wa uchaguzi wa rais hatua ambayo anasema wakili huyo ilikiuka sheria.
Underwood amesema pamoja na makosa mengine, mfuko wa wakfu huo ulitumika kwa ajili ya kufadhili kampeni ya uchaguzi yaTrump na hivyo kutumia vibaya kipengele cha kusamehewa kulipa kodi, pia wakfu huo ulitumika kwa ajili ya kulipia gharama za mahakami za Donald Trump na kutumia michango ya fedha iliyotolewa kwa shirika hilo kwa ajili ya kuendeleza biashara za Trump ikiwa pamoja na hoteli zake na kununulia vitu vyake binafsi. Mwanasheria Babra Underwood alifungua mashtaka dhidi ya Trump na watoto wake waliofikia umri wa utu uzima ikiwa ni pamoja na mshauri wa ikulu Ivanka Trump, kufuatia uchunguzi wa miezi 21 uliolenga shughuli za wakfu huo na jinsi ulivyojihusisha na kampeni ya urais ya Donald Trump.
Underwood amesema huu ni ushindi muhimu kwa utawala wa sheria, na umeonyesha kwamba kuna kanuni moja ya sheria kwa kila mtu. Amesema wataendelea mbele na mashtaka ili kuhakikisha kwamba dhidi ya wakfu huo wa Trump na wakurugenzi wake wanawajibishwa kutokana na vitendo vyao vya kukiuka waziwazi sheria za serikali mara kwa mara.
Wakati ambapo wakfu huo umekubali kujivunja bado lakini hatua hiyo inahitaji kuthibitishwa na hakimu. Hata hivyo Underwood anatafuta kurejeshwa kwa mamilioni ya dola na adhabu. Pia anataka kuwazuia rais Trump na watoto wake watatu wakubwa wasitumikie kwenye bodi zingine za misaada katika jimbo la New York. Mwanasheria anayeutetea wakfu wa hisani wa rais Trump amesema wakfu huo umetoa ufadhili wa takriban dola milioni 19 kwa zaidi ya mashirika 700 ya kutoa misaada.
Mwandishi: Zainab Aziz/p.dw.com/p/3AL1b
Mhariri: Mohammed Khelef