Wajumbe wa Urusi na Ukraine wawasili Uturuki kwa mazungumzo
15 Mei 2025Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, Maria Zakharova akizungumza Alhamisi na waandishi habari, amesema ujumbe wa Urusi umeshawasili Istanbul kuhudhuria mazungumzo hayo ya kwanza yanayofanyika ana kwa ana kwa zaidi ya miaka mitatu, na uko tayari kwa kazi kubwa.
Kulingana na Zakharova, ujumbe wa Urusi unaongozwa na Vladmir Medinsky msaidizi wa Putin. Ujumbe huo unawahusisha maafisa wengine watatu wa ngazi ya juu. Putin pia amewateua maafisa wengine wanne wa ngazi ya chini kama wataalamu wa mazungumzo hayo. Hata hivyo, Rais wa Urusi Vladmir Putin hatohudhuria mazungumzo hayo, licha ya viongozi wengi duniani kumtaka ahudhurie.
Afisa wa ngazi ya juu ya Ukraine amesema katika ujumbe wa Ukraine yumo pia Waziri wa ulinzi, Rustem Umerov, Waziri wa Mambo ya Nje, Andrii Sybiha, na mkuu wa Ofisi ya Rais, Andriy Yermak.
Mazungumzo yasogezwa mbele
Hata hivyo, Zakharova amesema mazungumzo hayo kati ya Urusi na Ukraine mjini Istanbul yamesogezwa mbele hadi alasiri. Zakharova amesema kuwa hatua hiyo imechukuliwa kutokana na ombi lililotolewa na upande wa Uturuki. Ukraine haijataja muda kamili wa mazungumzo hayo yanayosubiriwa kwa hamu kubwa.
Hatua ya Putin kutohudhuria mazungumzo hayo imekosolewa na maafisa wa mataifa ya Magharibi ambayo yamesema kwamba Urusi haizingatii kwa umakini kuhusu juhudi za amani. Rais Zelensky amesema hawakupewa taarifa rasmi kuhusu watu watakaohudhuria mkutano huo kutoka upande wa Urusi.
Aidha, ofisi ya Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan imesema kuwa kiongozi huyo atasisitiza katika mazungumzo na Rais Zelensky mtazamo wa Uturuki kwamba kunapaswa kuwepo mazungumzo ya kusitisha mapigano na upatikanaji wa amani bila kuchelewa ili kumaliza vita na Urusi.
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Rais, Fahrettin Altun ameandika katika mtandao wa kijamii wa X kwamba Erdogan atajadiliana na Zelensky masuala yote ya maendeleo yaliyofikiwa hivi karibuni katika vita vya Urusi na Ukraine. Zelensky amesema Ukraine itaamua kuhusu hatua zinazofuata katika mazungumzo na Urusi baada ya mkutano wake na Erdogan.
Trump huenda akahudhuria mazungumzo ya Uturuki
Wakati huo huo, Rais wa Marekani Donald Trump, amesema Alhamisi kuwa huenda akasafiri kwenda Uturuki kuhudhuria mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Urusi na Ukraine yenye lengo la kuvimaliza vita vya zaidi ya miaka mitatu ikiwa hatua zitapigwa.
Akizungumza akiwa ziarani Qatar, Trump amesema kama kutakuwa na maendeleo yoyote anaweza kuelekea Uturuki kesho Ijumaa. Awali Trump alisema angeenda Uturuki, iwapo Rais Putin angehudhuria mazungumzo hayo.
Soma zaidi: Trump atafakari kuhudhuria mazungumzo ya Uturuki
Akizungumza katika mkutano wa Jumuia ya Kujihami ya NATO ambao unafanyika pia nchini Uturuki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan amesema baada ya miaka mitatu ya mateso, hatimaye kuna dirisha la fursa ambalo limefunguliwa. Kulingana na Fidan, ana matumaini kuwa mazungumzo ya Istanbul yanaweza kufungua ukurasa mpya.
(AFP, AP, Reuters)