Wajumbe wa Urusi na Ukraine wakutana Instanbul
2 Juni 2025Kabla tu ya kuanza kwa mazungumzo hayo, Ukraine ilifanya moja ya operesheni zake za kijeshi za ujasiri zaidi kwa kushambulia maeneo ya ndani ya Urusi na kuharibu zaidi ya ndege 40 za kivita za kimkakati, ambazo thamani yake inakadiriwa kufikia dola bilioni 7. Ndege hizo zilikuwa zimeegeshwa katika vituo vya jeshi vya ndani kabisa, mbali na mstari wa mbele.
Idara ya ujasusi ya Ukraine imefichua kuwa mashambulizi dhidi ya ndege za Urusi yalikuwa sehemu ya mpango wa siri wa miezi 18, ambapo droni ziliingizwa kwa siri ndani ya Urusi na kurushwa kutoka maeneo ya ndani, jambo linaloonesha maendeleo makubwa ya uwezo wa mashambulizi ya mbali wa Ukraine.
Mtaalamu wa anga wa Ukraine, Valeriy Romanenko, aliisifu operesheni hiyo kama hatua muhimu ya mabadiliko.
Urusi na Ukraine kufanya mazungumzo Istanbul
"Ningependa kuona nyuso za wajumbe wa Urusi katika meza ya mazungumzo. Wangenifurahisha sana. Si mimi tu, bali kila mtu pia. Baada ya kofi hilo mbele ya macho ya dunia nzima, wanawezaje kufika na kusema, 'Hatutaki mikoa minne tu, tunataka sita?" alisema Romanenko.
Wakati huo huo, Urusi na Ukraine zilishambuliana Kwa droni usiku kucha. Urusi ilidai kudungua droni 162 za Ukraine, nyingi zikidunguliwa katika mikoa ya mpakani ya Kursk na Belgorod. Ukraine nayo ilisema ilizuia droni 80 za Urusi pamoja na makombora manne, ingawa baadhi yalifikia shabaha zake katika miji ya Kharkiv na Kherson.
Mazungumzo yanafanyika huku mapigano yakiendelezwa
Licha ya kurejea kwa mazungumzo, mapigano ya kijeshi yanaendelea kwa kasi. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alieleza masharti ya Kyiv kabla ya mazungumzo: kusitishwa kwa mapigano mara moja na bila masharti, kuachiliwa kwa wafungwa, na kurudishwa kwa watoto waliotekwa. Pia alisisitiza tena wito wake wa kufanyika kwa mkutano wa ana kwa ana na Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Wajumbe wa Urusi wamewasili Istanbul wakiwa na hati rasmi ya mapendekezo yao ya amani, ikiwa ni pamoja nakupunguzwa kwa uwezo wa kijeshi wa Ukraine, uthibitisho wa kutojiunga kamwe na Jumuiya ya NATO, na kukubali kupoteza maeneo ya ardhi. Kyiv na washirika wake wa Magharibi wamekataa masharti hayo wakiyaita ya kikoloni na yasiyokubalika.
Ujumbe wa Urusi unawakilishwa na Vladimir Medinsky, mshauri wa karibu wa Putin na mwenye historia tata, huku upande wa Ukraine ukiongozwa na Waziri wa Ulinzi Rustem Umerov. Wajumbe wa kidiplomasia kutoka Ujerumani, Ufaransa, na Uingereza pia wamewasili Istanbul kuisaidia timu ya Ukraine.
Licha ya hatua za kidiplomasia na mafanikio ya kijeshi, amani ya muda mrefu bado haijapatikana. Kyiv inakiri kuwa huenda ikalazimika kutegemea mazungumzo kurejesha maeneo yaliyopotea, lakini inasisitiza kuwakusitishwa kwa mapigano lazima kuambatane na dhamana za kiusalama kutoka kwa mataifa ya Magharibi - jambo ambalo Urusi bado inapinga.