Wajumbe wa Urusi na Ukraine wakutana Istanbul
23 Julai 2025Wajumbe wa Urusi na kutoka Ukraine wanakutana mjini Istanbul kwa mazungumzo ya moja kwa moja ya duru ya tatu, kujaribu kutafuta makubaliano ya kumaliza vita nchini Ukraine.
Urusi ambayo imethibitisha kwamba wajumbe wake tayari wameshafika Istanbul, imesema kuna mengi ambayo yatabidi kushughulikiwa kabla ya hata kufanyika majadiliano kuhusu uwezekano wa mazungumzo kati ya rais Putinna Zelensky ambao walikutana mara ya mwisho mnamo mwaka 2019.
Moscow imejizuia kuweka matumaini juu ya kupatikana mwafaka kupitia mazungumzo ya baadae leo mjini Istanbul kati ya pande hizo mbili, baada ya takriban miaka mitatu na nusu ya vita. Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov, alipoulizwa na waandishi habari kuhusu matarajio ya Moscow kwenye mazungumzo hayo alikuwa na haya.
"Bila shaka ni vigumu kuzungumzia kuhusu hili kwa sasa. Tutabidi tutazame namna mazungumzo yatakavyokwenda. Hapana shaka hakuna anayetarajia itakuwa kazi rahisi. Ni mazungumzo yatakayokuwa magumu. Rasimu za mapendekezo zinatofautiana kabisa''
Mazungumzo ya Istanbul ni ya duru ya tatu ya moja kwa moja kati ya wajumbe wa Ukraine na Urusi baada ya pande hizo kukutana katika mji huo Mei na Juni mwaka huu lakini zikashindwa kufikia makubaliano katika masuala kadhaa muhimu, na badala yake zilifanikiwa kukubaliana kubadilishana wafungwa wa kivita na miili ya wanajeshi waliouwawa vitani.
Rais Donald Trump wa Marekani wiki iliyopita akatowa muda wa siku 50 wa kuitaka Urusi imalize vita vyake hivyo nchini Ukraine la sivyo ikabiliwe na vikwazo.
Hata hivyo hakuna dalili kwamba serikali ya Urusiiko tayari kuachana na madai yake na ndiyo maana inasema majadiliano ya leo hayawezi kuwa rahisi.
Madai ya Urusi
Urusi inaitaka Ukraine iondoke kabisa katika majimbo manne inayodai iliyanyakuwa Septemba 2022, lakini Ukraine inasema pendekezo hilo la Urusi halikubaliki.Ukraine nayo imekataa kufanya mazungumzo yoyote kuhusiana na suala la ardhi yake iliyonyakuliwa na Urusi mpaka usitishaji vita ufanyike.
Pamoja na hayo imekuwa ikitarajia kwamba Urusi itakubali kuitisha mkutano kati ya Rais Vladmir Putin na Volodymyr Zelensky na kufikiwa makubaliano ya kumaliza vita. Lakini pande hizo mbili zinatofautiana kabisa kimisimamo juu ya namna ya kuvimaliza vita hivyo.
Pamoja na kuweko tafauti hizo, rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amekuwa akizitolea mwito pande hizo mbili kutoufunga mlango wa mazungumzo.
Na wakati ikisubiriwa kuona kitakachotokana na duru hiyo mpya ya mazungumzo ya Istanbul, Urusi haijaacha kuishambulia Ukraine. Wizara yake ya ulinzi imesema hivi leo kwamba vikosi vyake vimekiteka kijiji kimoja katika mkoa wa Kaskazini mwa Ukraine wa Sumy.
Wakati huohuo Ukraine kwenyewe kadhia iliyojitokeza ya rais Zelensky kubinya uhuru wa mashirika mawili ya kukabiliana na rushwa imeibuwa sauti za kumkosoa Zelensky ndani na nje ya nchi hiyo.
Mkuu wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amemtaka kiongozi huyo kutowa ufafanuzi kuhusu uamuzi wake wa kufanya mabadiliko ya kuufuta uhuru wa mashirika ya kupambana na rushwa.