Wajumbe wa Ukraine na Urusi wako Uturuki kujadili amani
15 Mei 2025Rais wa Urusi Vladmir Putin hakuwa sehemu ya ujumbe wa Moscow. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami NATO Mark Rutte amesema ana matumaini lakini kwa tahadhari kuhusu kupatikana amani, akisema ni juu ya Urusi kuchukua hatua zinazofuata
Soma pia: Zelensky amtolea mwito Trump kuhakikisha mkutano kati yake na Putin unafanyika
"Ni wazi kwamba Urusi sasa inatuma ujumbe wa ngazi ya chini nchini Uturuki, kwa mazungumzo haya ya amani. Ni WaUkraine ambao wamesema, tuko tayari kukaa meza moja na Warusi, kukubaliana kusitisha mapigano, ili kuingia mara moja katika mazungumzo kuhusu hatua zinazofuata za kumaliza vita hivi vya kutisha."
Maelezo kuhusu ni wapi na wakati gani ujumbe wa Ukraine huenda ukakutana na wenzao wa Urusi bado hayajafahamika. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, Maria Zakharova amesema mazungumzo hayo kati ya Urusi na Ukraine mjini Istanbul yamesogezwa mbele hadi alasiri. Zakharova amesema kuwa hatua hiyo imechukuliwa kutokana na ombi lililotolewa na upande wa Uturuki. Ukraine haijataja muda kamili wa mazungumzo hayo yanayosubiriwa kwa hamu kubwa.