Wajumbe wa Taliban wako Ujerumani kuratibu safari za ndege
22 Julai 2025Serikali ya Ujerumani imesema wajumbe wawili wapya wametumwa na utawala wa Taliban nchini Afghanistan kusaidia kuratibu mchakato wa kuwarejesha kwao raia wa nchi hiyo, baada ya Wafghani 81 waliotiwa hatiani kurejeshwa katika nchi yao.
Safari yao iliyofanyika Ijumaa wiki iliyopita ilikuwa ya pili kutokea Ujerumani tangu kuwafukuza raia wa Afghanistan kulipoanza tena mwaka uliopita. Ujerumani haiwatambui viongozi wa Taliban nchini Afghanistan lakini ina mawasiliano ya kiufundi kuhusiana na safari za kuwarejsha kwao raia wa Afghanistan, ambazo zimeratibiwa na Qatar.
Msemaji wa serikali ya Ujerumani Stefan Kornelius amesema wakati wa mabadilishano imekubaliwa kwamba wajumbe hao wawili wa utawala wa Afghanistan watajumuishwa katika ubalozi mdogo wa Afghanistan nchni Ujerumani.
Duru katika wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imelithibitisha shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba wajumbe hao waliwasili Ujerumani wikendi iliyopita.