Wajerumani wachagua uongozi mpya katika uchaguzi muhimu
23 Februari 2025Wajerumani wanaendelea kupiga kura leo katika uchaguzi wa wabunge ambao uliitishwa mapema baada ya muungano wa chama tawala cha SPD chake Kansela Olaf Scholz kusambaratika mwezi Novemba. Mgombea wa upinzani wa chama cha CDU Friedrich Merz anapewa nafasi kubwa ya kuwa kansela ajaye, huku kambi ya kihafidhina inayojumuisha chama cha CSU ikitarajiwa kupata karibu asilimia 30.
Soma: Nani atakuwa Kansela mpya wa Ujerumani?
Chama cha mrengo mkali wa kulia cha AfD kiko nafasi ya pili kwa takriban asilimia 20 ya uungwaji mkono, kulingana na tafiti za kabla ya uchaguzi. Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amewahimiza raia kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo la upigaji kura kwa mustakabali wa taifa hilo.
"Uchaguzi ndio msingi wa demokrasia yetu. Bila uchaguzi huru na haki hakuwezi kuwa na demokrasia. Kwa mantiki hiyo nawasihi kwenda kupiga kura. kapige kura. Saidia kuamua mustakabali wa nchi yetu. Piga kura ukijua kura yako inaweza kuleta mabadiliko", aliongeza rais Steinmeier. Vituo vya kupigia kura vitafungwa saa 12 jioni kwa saa za hapa Ujerumani.