Wahouthi wavamia ofisi za UN Yemen, wafanyakazi wakamatwa
31 Agosti 2025Wahouthi wamevamia ofisi za mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayoshughulika na chakula na watoto mjini Sanaa, Yemen, na kuwakamata wafanyakazi wasiopungua 11, huku vikosi vyao vikiimarisha ulinzi kufuatia kuuawa kwa waziri mkuu na mawaziri kadhaa katika shambulizi la anga la Israel wiki iliyopita.
Msemaji wa Shirika la Chakula Duniani (WFP), Abeer Etefa, alisema vikosi vya usalama vilivamia ofisi hizo Jumapili asubuhi na kusisitiza kuwa "kukamatwa kiholela kwa wafanyakazi wa misaada ni jambo lisilokubalika.”
Mashirika mengine yaliyoathirika ni pamoja na UNICEF, huku mawasiliano na wafanyakazi kadhaa yakikatika, ishara kwamba huenda nao wamekamatwa.
Msemaji wa UNICEF, Ammar Ammar, alithibitisha kuwa kuna "hali inayoendelea” kuhusiana na ofisi zao mjini Sanaa lakini hakutoa maelezo zaidi.
Raia wa eneo hilo wamesema hatua hii ni mwendelezo wa msako mkali wa muda mrefu wa Wahouthi dhidi ya mashirika ya kimataifa yanayofanya kazi katika maeneo wanayoyadhibiti.
Mashirika ya misaada na wafanyakazi wa balozi za kigeni, ikiwemo ya Marekani, yamewahi pia kuripoti unyanyasaji na ukamataji wa mara kwa mara.
Mwezi Januari, Umoja wa Mataifa ulilazimika kusitisha shughuli zake katika ngome ya Wahouthi ya Saada baada ya wafanyakazi wanane wa shirika hilo kukamatwa. Hadi sasa, makumi ya wafanyakazi wa mashirika ya kimataifa na ya kiraia wanashikiliwa bila mashtaka rasmi.
Viongozi wakuu wa Wahouthi wauawa na Israel
Uvunjaji huo wa ofisi za mashirika ya kimataifa umefuatia shambulizi kubwa la anga la Israel lililowaua viongozi kadhaa waandamizi wa Wahouthi, akiwemo Waziri Mkuu Ahmed al-Rahawi, pamoja na mawaziri wa Mambo ya Nje, Nishati, Utalii, Habari, na Maendeleo ya Mitaa.
Miongoni mwa waliouawa pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Abdel-Majed al-Murtada, mmoja wa maafisa wenye ushawishi mkubwa katika kundi hilo.
Shambulizi hilo, kwa mujibu wa taarifa ya Wahouthi, liliwalenga viongozi waliokuwa kwenye warsha ya kawaida ya tathmini ya kazi za serikali.
Mazishi ya viongozi hao yamepangwa kufanyika Jumatatu katika Uwanja wa Sabeen, katikati mwa Sanaa.
Waziri wa Ulinzi Mohamed Nasser al-Attefi alinusurika shambulizi hilo, huku Waziri wa Mambo ya Ndani Abdel-Karim al-Houthi, mmoja wa watu wenye nguvu zaidi ndani ya kundi hilo, akisemekana kuwa hakuwepo kwenye kikao kilicholengwa.
Mashambulizi ya Wahouthi yatarajiwa kuongezeka
Shambulizi la Israel lilikuja baada ya Wahouthi kurusha kombora la masafa marefu mnamo Agosti 21, ambalo jeshi la Israel lilisema lilikuwa bomu la mtawanyiko lililolenga Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion.
Mashambulizi hayo yalizua taharuki, yakisababisha milio ya kengele za tahadhari kusikika katikati ya Israel na Jerusalem, na mamilioni ya raia kukimbilia hifadhi.
Katika hotuba yake ya Jumapili, kiongozi msiri wa kundi hilo Abdul-Malik al-Houthi alisema mashambulizi ya makombora, droni, na mzingiro wa baharini dhidi ya Israel "vitaendelea kwa kasi na kuongezeka,” akisisitiza kwamba kampeni hiyo inalenga kushinikiza Israel kukomesha vita vya Gaza.
Wataalamu wa usalama wanaonya kuwa hali hii inaweza kuongeza mashambulizi ya Wahouthi dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari ya Shamu, hasa kufuatia tishio lao la Julai kwamba meli za kampuni yoyote inayoshirikiana na bandari za Israel zitakuwa shabaha, bila kujali taifa la usajili wake.
Hali hii inatishia kuongeza mgogoro wa kibinadamu katika eneo ambalo tayari linakabiliwa na njaa, vita vya muda mrefu, na ukosefu wa msaada wa kutosha kwa mamilioni ya raia waliokwama katikati ya mapigano.
Chanzo: AP