Wahouthi: Shambulio la Marekani limewaua wahamiaji 68 Yemen
28 Aprili 2025Taarifa ya Wahouthi iliyotolewa mapema Jumatatu , imesema kando ya watu 68 waliouwawa katika shambulio hilo kwenye eneo la Saada, watu wengine 47 wamejeruhiwa. Kwa mujibu wa waasi hao wa Yemen, wahamiaji 115 walikuwa wakishikiliwa kwenye kituo hicho wakati wa shambulio hilo. Eneo lililoshambuliwa linafahamika kuwa ngome kubwa ya waasi hao.
Soma zaidi: Marekani yaendeleza mashambulizi dhidi ya waasi wa Kihouthi huko Yemen
Kituo cha televisheni cha Al Masirah chenye mfungamano na waasi wa Kihouthi kimeripoti kuwa shughuli za uokoaji na timu za huduma za dharura zinakabiliwa na changamoto kutokana na uharibifu mkubwa uliotokana na shambulio hilo. Picha za video zilizotolewa na kituo hicho zimeonesha kile kilichoonekana kuwa miili ya waliouwawa na watu waliojeruhiwa wakiwa katika eneo la tukio. Picha nyingine zilizotolewa baadaye zimewaonesha majeruhi wakipatiwa matibabu hospitali.
Wizara ya mambo ya ndani iliyo chini ya serikali ya Wahouthi ambayo haitambuliwi kimataifa imelaani shambulio hilo iliyoliita kuwa"uhalifu wa kutisha uliofanywa na Marekani kwa kulenga kituo cha wahamiaji wasio na vibali kutoka Afrika"
Kituo kilichoshambuliwa kilisimamiwa na IOM
Kulingana na Wizara hiyo, kituo hicho kilikuwa chini ya usimamizi wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM na Shirika la Msalaba Mwekundu. Zaidi imeongeza kuwa wengi wa wahamiaji wa Kiafrika waliokuwemo kwenye kituo kilichoshambuliwa ni kutoka Ethiopia ambao mara nyingi hufunga safari hatari kupitia Yemen kwenda Saudi Arabia wanakotumaini kupata kazi na maisha bora.
K abla ya habari za shambulio hilo kutolewa, Kamandi kuu ya Marekani ilitoa taarifa iliyolenga kuitetea sera yake ya kutokutoa maelezo mahsusi kuhusu mashambulizi yake makubwa ya anga.
Mashambulizi yanayofanywa na Marekani yameibua utata kuhusu Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo Pete Hegseth kutumia programu ya kutuma na kupokea ujumbe ya Signal kuwasilisha taarifa za siri kuhusu mashambulizi.