Wahamiaji 68 wa Kiafrika wafa maji Yemen
4 Agosti 2025Mashua hiyo iliyokuwa imebeba wahamiaji 154, wengi wao wa jamii ya Oromo kutokea Ethiopia, ilizama kwenye Ghuba ya Aden, kusini mwa jimbo la Abyan, mapema siku ya Jumapili (Agosti 3).
Mkuu wa IOM nchini Yemen, Abdusattor Eusov, aliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba miili 54 ilisombwa na maji hadi katika wilaya ya Khanjar, ambapo miili mingine 14 ilipelekwa kwenye hospitali ya mji mkuu wa jimbo hilo, Zinjibar.
Kwenye ripoti yake, idara ya usalama ya jimbo la Abyan ilisema operesheni kubwa ya msako na uokoaji ilikuwa inaendelea kutokana na idadi kubwa ya waliofariki dunia na wale wasiojuilikana walipo.
Operesheni hiyo ilikuwa inawajumuisha pia wavuvi na wanavijiji, huku miili ikiripotiwa kutawanyika kwenye eneo pana la fukwe za Abyan.
Abdul-Qadir Bajameel, afisa wa afya wa jimbo hilo, alisema ni watu 10 tu kati ya 154 waliokuwamo kwenye mashua hiyo ndio walioweza kuokolewa, ambapo tisa walikuwa Waethiopia na mmoja Myemen.
Yemen lango la wahamiaji wanaokimbilia Arabuni
Licha ya zaidi ya muongo mmoja wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, Yemen bado imesalia kuwa njia kuu kwa wahamiaji kutoka mataifa ya Mashariki na Pembe ya Afrika wanaojaribu kuyafikia mataifa ya Ghuba ya Arabuni, hasa Saudi Arabia na Umoja wa Falme wa Kiarabu, kusaka kazi za vibarua.
Wahamiaji hao huwa wanasafirishwa na walanguzi kupitia njia za hatari, kama vile ujia wa Bab al-Mandab unaozitenganisha Djibouti na Eritrea kutoka Yemen, wakiwa kwenye mashua zilizojaa watu, wakikimbia vita na umasikini kwenye mataifa yao.
Maelfu ya wahamiaji hao ama wamekufa maji au kupotea wakiwa kwenye mashua hizo mbovu katika miezi ya hivi karibuni.
IOM iliutaja mwaka 2025 kuwa mmojawapo wa miaka yenye idadi kubwa zaidi ya wahamiaji.
Kabla ya ajali hiyo ya Jumapili, ajali mbaya zaidi ya karibuni kabisa ilikuwa ile ya mwezi Machi, ambapo wahamiaji wawili walithibitishwa kupoteza maisha na wengine 186 kupotea baada ya mashua zao nne kuzama kwenye pwani za Yemen na Djibouti.
Ripoti ya IOM ilisema zaidi ya wahamiaji 60,000 waliwasili nchini Yemen mnamo mwaka 2024, wakiwa pungufu ya wahamiaji 97,200 mwaka 2023, huenda kwa sababu wakati huo kulikuwepo doria ya walinzi wa pwani.
Shirika hilo linasema makumi kwa maelfu ya wahamiaji bado wamekwama katika taifa hilo masikini kabisa katika Bara Arabu, ambako wanakabiliwa na shida kadhaa, zikiwemo njaa, maradhi na hali mbaya zaidi ya kibinaadamu.
//AP, Reuters