Wageni wanaoishi kinyume cha sheria Ujerumani.
30 Septemba 2004Kuna Wageni wapatao kati ya Laki tano na millioni moja wanaoishi Ujerumani kinyume cha sheria. Ili wasiweze kukamatwa na kurudishwa makwao hutembea kwa tahadhari kubwa. Mambo huenda vizuri ikiwa hawatapatikana na janga kama vile makosa, ajali au ugonjwa. Hali kama hiyo, mara kwa mara, hutumiwa vibaya.
Rais wa Shirika la Caritas nchini Ujerumani, Peter Neher, analalamika kwa kusema, "Sekta nyingi za kibiashara kama vile ujenzi, hoteli, kilimo, usafishaji na pia hata kazi za nyumbani huwatumia watu hao bila ya kugharamia bima zao za afya. Isitoshe, Wafanyakazi hao wasiokuwa halali wanalazimika kuishi katika mazingara mabaya na hata kupewa kazi ngumu."
Padre Alborino wa Idara ya kuwahudumia Wakimbizi ya Jesuit anasema kuwa Wageni wanaoishi kinyume cha sheria wanaweza kuishi muda mrefu kwa kujificha lakini matatizo yatatokea iwapo watapata ajali au watakuwa wagonjwa.
Padre Alborino anasema, "Mara nyingi inahusu Wanawake waja wazito ambao hawapati huduma za tiba. Hapa ina maanisha kuwa uchunguzi wa kina unaopaswa kufanywa na Madaktari au hospitali ambazo ziko tayari kuwasaidia Wanawake hawa bila ya gharama yo yote ile. Hapa Kanisa Katoliki linaweza kusaidia kama liwezavyo."
Ingawaje serikali ina haki ya kuwakamata watu hao na kuwarudisha makwao lakini lazima kwanza utu uwekwe mbele.
Padre Jorg Alt wa Idara ya kuwahudumia Wakimbizi ya Jesuit anasema, "Siku zote tunasema kuwa sheria za Wageni na haki ya kila mtu kuishi maisha bora ni masuala mawili yaliyo tofauti kabisa na ya haki. Lakini lazima ukatili usitumiwe wakati Wageni wanaoishi kinyume cha sheria wanapogunduliwa na kukamatwa."
Padre Alt anasema kuwa kila mtu ana haki ya kulindwa. Haya yamo ndani ya katiba na yamepewa kipaumbele. Hata ikiwa mtu huyo anaishi kinyume cha sheria ana haki ya kupata mahali pa kuishi na hata matibabu.
Padre Alt anasema, "Tatizo siyo kuwapata Madaktari, kuna Madaktari wa kutosha. Tatizo kubwa ni gharama zinazoambatana na matibabu yenyewe kama vile uchunguzi unaofanywa na Maabara, kulazwa hospitalini na matibabu ya muda mrefu. Wengi wanaokuja kwetu ni Wajawazito wasiopenda kutoa mimba na wanakuja Kanisani na kuomba ushauri wafanye nini ili mtoto azaliwe. Haya ndiyo matatizo yaliyojitokeza tokea miaka michache iliyopita."
Ndiyo maana Kanisa Katoliki sasa linataka kuzungumza na Wanasiasa. Linataka hata wale wanaoishi kinyume cha sheria nchini Ujerumani wawe na maisha bora na kuwe na sheria za kuwazuia wasinyonywe. Wanawake wengi wanalazimishwa kuwa Malaya na hawana uwezo wa kujikomboa tena.
Rais wa Shirika la Caritas nchini Ujerumani Peter Neher anataka Wageni wanaoishi kinyume cha sheria wawe na Mtetezi wao.
Anasema, "Nchi jirani zimekwenda mbali mno. Mada hiyo imewekwa katika ajenda ya Wananchi tokea miaka kadhaa iliyopita."
Padre Jörg Alt ana lalamika kwa kusema kuwa ingawaje ni hivyo kuna mvutano wa kisiasa nchini Ujerumani. Chama peke yake ambacho kiko tayari kusikiliza na kuchukua hatua ni kile cha Walinzi wa Mazingira. Jambo la kushangaza ni kuona kuwa upinzani mkubwa unatoka katika vyama vya Kikristo vya Christian Democratic (CDU) na Christian Social (CSU).