Wafugaji Tanzania wadaiwa kutumia ARV kukuza mifugo
10 Aprili 2025Katika jiji la Dar es Salaam, kila baada ya hatua kadhaa, utakutana na kibanda cha wauza chipsi, mayai, kuku na hata maeneo ya kuuza nyama ya nguruwe iliyokaangwa, iliyochomwa ama iliyowekwa pilipili kwa wingi maarufu kama makange. Haya ndiyo maisha ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam.
Lakini huenda wengi hawajui kilichojificha nyuma ya pazia katika nyama hizi wanazokula, kwani utafiti uliochapishwa Desemba 30 mwaka 2024, ulibaini kuwa, wafugaji walio wengi katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya na Iringa, wanatumia dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi,-ARV ili kunenepesha, kutibu magonjwa na kuchagiza utagaji wa mayai kwa kuku na kuongeza uzaaji wa nguruwe.
Utafiti huo ulifanywa na Chuo Kikuu Shirikishi cha Afya, (MUHAS) kwa kushirikiana na Dk Zuhura Kimera na wenzake na kuchapishwa na jarida la Afya la utafiti. Maafisa kilimo, wafugaji na wauzaji wa dawa za mifugo 113 katika wilaya nane za mikoa ya Mbeya, Iringa na Dar es Salaam, walihojiwa kuanzia Februari hadi Mei, 2023.
Zipi athari za kula nyama ya mifugo iliyopewa ARV
Watafiti hao walihitimisha kwa kusema kuwa maafisa kilimo na wafugaji katika maeneo hayo ya utafiti walithibitisha kutumia au kushuhudia wafugaji wakitumia ARV na dawa za uzazi wa mpango kwa Wanyama. Akizungumzia kuhusu utafiti huo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani ya Mwili, kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Elisha Osati ameyataja madhara ya kula wanyama waliopewa vidonge vya kufubaza maamkubikizi ya virusi vya Ukimwi- ARV, ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mazingira kutokana na vinyesi vya wanyama hao kutapakaa na kuleta pia madhara kwa wagonjwa wanaotumia dawa hizoambao inaweza kusababisha usugu wa dawa.
Hayo yakielezwa, tafiti nyingine zinaonyesha kuwa, ulaji wa nyama ya nguruwe unatarajia kuongezeka kutoka tani 42.7 hadi tani 170 ifikapo mwaka 2030, kuanzia mwaka 2017. Vilevile, makadirio yanaonyesha kuwa uzalishaji wa kuku kwa mwaka umeongezeka kutoka tani 22,000 mwaka 2017 hadi tani 37,200 mwaka 2023. Taarifa za utafiti huu zimewashtusha watanzania walio wengi ambao baadhi wameonyesha wasiwasi wao kuhusu matumizi hayo ya ARV kwa wanyama wanaokula karibu kila siku.
Katika utafiti huo, imeelezwa kuwa, wafugaji wanatumia dawa za ARV ili kuwanenepesha wanyama hao lakini pia kutibu magonjwa kama homa ya nguruwe, maarufu kama Swine Flu na ugonjwa mafua na kuharisha kwa kuku. Sababu zinazotajwa kuwa chanzo kwa wafugaji hao kutumia ARV kwa Wanyama hao ni pamoja na kujipatia faida, ushindani katika masoko, na ushauri wa maafisa mifugo.