MSF: "Wafanyakazi wetu waliuliwa kwa makusudi" Ethiopia
15 Julai 2025Shirika hilo aidha limeishutumu serikali ya Ethiopia kwa kushindwa "kutimiza wajibu wake wa kimaadili" wa kukamilisha uchunguzi.
Jimbo la Tigray lililopo kaskazini mwa Ethiopia liliingia kwenye vita vibaya kabisa vya raia dhidi ya serikali ya shirikisho kati ya mwaka 2020 na 2022 na kusababisha vifo vya karibu watu 600,000.
Machafuko hayo yalisababisha mzozo wa kibinaadamu huku watu milioni moja wakiwa hawana makaazi. Makubaliano tete ya amani nayo hayafanya chochote zaidi ya kusababisha chuki kubwa miongoni mwa jamii.
Waliouawa walikuwa ni Maria Hernandez, raia wa Uhispania, 35 aliyekuwa mmoja ya waratibu wa huduma za dharura huko Tigray, na wasaidizi wake Yohannes Halefom Reda na Tedros Gebremariam Gebremichael, wote wenye umri wa miaka 31.
Watumishi wa MSF waliuliwa kwa kupigwa risasi
Watumishi hao wa MSF-Uhispania waliuawa kwa kupigwa risasi Juni 24, 2021 kusini mwa Tigray na kulingana na shirika hilo magari yao yalikuwa yakitambulika.
"Hii imetuthibitishia kwamba shambulizi hilo lilikuwa mauaji ya kukusudia na yaliyowalenga wafanyakazi watatu wa misaada waliotambuliwa waziwazi," inasomeka taarifa ya MSF.
Kulingana na shirika hilo msafara wa wanajeshi wa Ethiopia ulikuwepo wakati wa shambulizi hilo.
MSF ilisema licha ya kufuatilia sana kwenye mamlaka ya shirikisho ya Addis Ababa bado hawajapata "majibu yoyote ya kuaminika" na serikali "imeshindwa kutekeleza majukumu yake ya kimaadili ya kukamilisha uchunguzi wa shambulizi hilo".
Ripoti hii inachapishwa baada ya uchunguzi wa kimataifa wa mwaka 2022 baada ya shirika hilo kusema wafanyakazi wake watatu waliuawa "kwa makusudi" bila ya kutoa maelezo zaidi.
Serikali na jeshi bado wako kimya
Gazeti la The New York Times la Marekani lilidai kwenye uchunguzi wa mwaka 2022 kwamba kanali mmoja wa Ethiopia aliagiza kuuliwa kwa wafanyakazi hao wa misaada, lakini mkurugenzi mkuu wa MSF-Uhispania amesema siku ya Jumanne kwamba "hawawezi kuthibitisha ama kwenda mbali kwa kiasi hicho".
Ripoti ya uchunguzi iliwasilishwa kwa mamlaka ambazo hata hivyo hazikuwa tayari kuizungumzia, limesema shirika hilo. Jeshi na mamlaka za shirikisho pia hazikuwa tayari kusema lolote lilipoombwa na shirika la habari la AFP.
Ethiopia, nchi ya pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika ikiwa na karibu wakaazi milioni 130, imekuwa ikiongozwa na Waziri Mkuu Abiy Ahmed tangu 2018.
Vikosi vya shirikisho pia vinashutumiwa kwa unyanyasaji katika mikoa miwili yenye watu wengi zaidi nchini humo ya Amhara na Oromia.