Wafadhili waahidi euro milioni 800 kwa ajili ya Sudan
16 Aprili 2025Nchi wahisani kutoka Ulaya na Afrika zimeahidi zaidi ya euro milioni 800 kwa ajili ya misaada ya kibinadamu kwa Sudan, katika kile kilichoelezwa kuwa ni juhudi za kukabiliana na janga baya zaidi la kibinadamu duniani kwa sasa.
Mkutano huo wa siku moja umefanyika jijini London huku Sudan ikiadhimisha miaka miwili tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mkutano huo uliandaliwa na Uingereza, Umoja wa Ulaya, Ufaransa, Ujerumani na Umoja wa Afrika, na ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi zaidi ya 15 na mashirika ya kimataifa, lakini hakuna upande wowote kutoka Sudan ulioshiriki – jambo lililozua mjadala mpana.
Vita vilivyoigawanya Sudan
Vita vilianza mnamo Aprili 15, 2023, baada ya mivutano kati ya jeshi la Sudan linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na vikosi vya RSF vinavyoongozwa na Mohamed Hamdan Daglo. Mapigano hayo sasa yamesababisha vifo vya maelfu, zaidi ya watu milioni 14 wamekosa makazi, na wengine milioni 3.5 wamekimbilia nchi jirani kama Chad na Misri.
Soma pia: London yaandaa mkutano kutafuta njia ya kumaliza vita Sudan
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, David Lammy, alitangaza msaada wa pauni milioni 120, akisisitiza kuwa ukosefu wa nia ya kisiasa ndicho kikwazo kikubwa zaidi: “Tunahitaji diplomasia yenye uvumilivu. Lazima tushawishi pande zinazozozana kuwalinda raia, kuruhusu misaada kuingia, na kuweka amani mbele.”
Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wake walihaidi euro milioni 522, Ujerumani euro milioni 125, na Ufaransa euro milioni 50 ya ziada kwa mwaka ujao.
Wasiwasi wa kugawanyika kwa taifa
Kamishna wa AU, Bankole Adeoye, alionya dhidi ya jaribio lolote la kugawanya Sudan: “Umoja wa Afrika hautakubali Sudan kugawanyika. Ni lazima tulinde umoja wa kisiasa, mipaka na mamlaka ya taifa.”
Onyo hilo lilikuja siku chache baada ya RSF kujitangaza kuunda “Serikali ya Amani na Umoja” katika maeneo wanayoyadhibiti, wakieleza kuwa wanafanya hivyo kwa kushirikiana na vyama vya kiraia.
Shirika la Chakula Duniani, WFP, limeripoti kuwa asilimia 50 ya wananchi wa Sudan wanakabiliwa na njaa kali, huku UN ikisema zaidi ya watu milioni 30 wanahitaji msaada wa dharura. Aidha, wanawake na watoto zaidi ya milioni 12 wako katika hatari ya ukatili wa kijinsia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock alisisitiza: Hakuna kiasi cha misaada kitakachotosha ikiwa vita vinaendelea. Vita hivi lazima vikome.”
Sauti ya kimataifa yasikika, lakini amani bado ni ndoto
Ingawa mataifa ya Magharibi yana nafasi ndogo ya kumaliza mapigano, mkutano huo uliitaka Misri na UAE, ambazo zina ushawishi mkubwa kwa pande husika, kutumia nafasi yao kuhimiza amani. Sudan imeituhumu UAE kwa kuisaidia RSF kwa silaha – tuhuma ambazo UAE imekanusha.
Soma pia: Vita vya Sudan miaka miwili baadae, hali bado ni mbaya
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot, alisema: “Wadau wa nje wanaoshiriki katika mzozo huu lazima waache kutoa msaada wa kijeshi. Umoja wa Sudan ni lazima udumishwe.”
Wakati wa maadhimisho haya ya miaka miwili ya vita, dunia inajitahidi kutoa misaada ya dharura – lakini hali halisi ya Sudan bado ni ya wasiwasi mkubwa. Hatua ya RSF kujitangazia serikali yao wenyewe imechochea hofu ya kugawanyika kwa taifa, huku wito wa kusitisha vita ukiendelea kupuuzwa.
“Tuna wajibu wa kimaadili – hatuwezi kuipuuza Sudan,” alisisitiza Lammy.