Wafadhili wa kimataifa wakata tamaa na hali ya Somalia
29 Julai 2025Kwa mujibu wa taasisi ya Umoja wa Ulaya ya uchunguzi wa usalama, tangu mwaka 2007 mataifa wafadhili ikiwemo yale ya Umoja huo na Marekani wamewekeza zaidi ya dola bilioni saba katika mipango mbalimbali ya Umoja wa Afrika ya kurejesha amani Somalia. Fedha hizo aidha zilisaidia katika kujenga jeshi la kitaifa la Somalia ambalo limendelea kukabidhiwa jukumu la kusimamia usalama wa nchi hiyo huku mchakato wa kuyaondoa majeshi ya kijeni ukiendelea.
Somalia na Marekani wawashambulia wapiganaji wa al-Shabaab
Lakini katika miezi ya hivi karibuni, wapiganaji wa Al Shabaab wamedhihirisha kujiimarisha na kuteka tena maeneo yaliyokuwa yamekombolewa. Kulingana na mchambuzi mmoja wa Somalia, sasa Al Shabaab wanadhibiti maeneo kutoka Kusini Magharibi hadi Kaskazini Magharibi ya Mogadishu yakikalia miji kadhaa ya kimkakati kiuchumi na kiusalama.
Tarehe saba mwezi huu wa Julai, Al Shabaab waliuteka tena mji wa Moqokori, katika mojawapo ya wimbi la kushindwa kwa jeshi la serikali. Hali hii imewavunja moyo wafadhili wa kimataifa na kulingana na mwanadiplomasia ambaye hakutaka kutajwa, mataifa wafadhili wanajiuliza kuhusu matokeo ya kuwekeza katika kujenga usalama na uthabiti wa Somalia katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Wanapata mashaka kutokana na ripoti kwamba wanajeshi wa Somalia husalimu amri na kuondoka mara tu Al Shaabab wanapofika.
Marekani ndiyo hasa inatafakari kama itaendelea kufadhili usalama Somalia. Lakini kwa baadhi ya wadadisi si ajabu kwamba Al Shabaab inawazidi nguvu wanajeshi wa Somalia. Msemaji wa jeshi la Uganda Brigedia Jenerali Felix Kulaigye anaelezea kuwa mapendekezo ya mataifa wafadhili na pia maamuzi ya Umoja wa Afrika kukabidhi mamlaka kwa jeshi la Taifa Somalia ambalo lingali changa yaliharakishwa bila kuzingatia uwezo wa jeshi hilo na pia kutochunguza ipasavyo uwezo wa Al Shabaab.
"Hatujashangaa. Umoja wa Ulaya na Marekani walikuwa na haraka bila kuzingatia viwango vya mafunzo kwa jeshi la Somalia. Sisi upande wetu hatujavunjika moyo."
Umoja wa Mataifa wawaomba wafadhili kuisaidia Somalia
Kulingana na Omar Mahmood wa Kundi la Kimataifa linalofuatilia mizozo, Al Shabaab sasa wako katika eneo la kimkakati kuweza kufanya mashabulizi katika kanda ya Hiiraan ambayo wapiganaji wa ki ukoo wa sehemu hiyo wamefanya juhudi kubwa kuilinda. Inasemekana kuwa katika harakati za kijeshi kati ya mwaka 2022 na 20233 serikali ilitegemea pakubwa wapigajani wanaojulika kama “Macwiisley” walipofanikiwa kuiteka zaidi na miji na vijiji 200 kutoka kwa Al Shabaab.
Lakini kutokana na kuibuka kwa mivutano ya kisiasa miongoni mwa viongozi wa nchi hiyo, usalama haujapewa kipaumbele na badala yake rais Mahmoud anadhani kuwa suala muhimu ni kuandaa uchaguzi mwaka ujao bila kuzingatia hali ya usalama kwenye vituo vya kupigia kura.
Watu 11 wauawa katika shambulizi la kigaidi Mogadishu
Aliyekuwa rais wan chi hiyo Sharif Sheikh Ahmed amewambia wandishi habari hivi karibuni kwamba ni jambo la kusikitisha kuwa utawala unayazingatia masuala ya kisiasa yasiyokuwa na umuhimu ambayo hayana uhusiano wowote na usalama wa kitaifa.Miji kama Masaajid Cali Gaduud na Adan Yabal, ambayo ilikuwa vielelezo vya uthabiti yote sasa iko mikononi mwa Al Shabaab.
Kwa sasa inadaiwa Al Shabaab wanadhibiti sehemu kubwa ya uchumi wa Somalia na kutajwa kuwa mojawapo ya wapiganaji matajiri barani Afrika. Serikali ya Somalia imebaini kwamba wafadhili wa Ulaya na Marekani wamezidi kuchoka kutoa misaada. Hivi karibuni serikali imejenga ubia na mataifa ya Milki wa Uarabuni, Qatar,Misri na Uturuki. Lakini ukweli ni kwamba mataifa hayo yanatanguliza maslahi yao, Uturuki imeleta wanajeshi 500 kulinda miradi yake ya uwekezaji.