WAFA: Wapalestina 89 wauawa Gaza
14 Agosti 2025Shirika la WAFA limeripoti kuwa karibu nusu ya waliouawa walikuwa wamesajiliwa katika mji wa Gaza. Kulingana na WAFA, watu saba waliuawa kaskazini magharibi mwa Mji wa Gaza katika kituo cha kusambaza misaada ya kiutu.
Walikuwa wamepelekwa huko kusaidia shughuli za kusambaza misaada. Watu wengine saba, wakiwemo watoto watano wameuawa baada ya shambulizi la anga kupiga katika hema lao kwenye Mji wa Gaza.
Waliouawa walikuwa wakisubiri msaada
Aidha, kwa mujibu wa duru za kitabibu, shambulizi jingine la droni limepiga kaskazini mwa Gaza na kumuua mtu mmoja. Katika shambulizi jingine la Israel, watu watano waliuawa wakati wakisubiri msaada kusini mwa eneo la Wadi Gaza.
Mashambulizi hayo yamefanyika wakati ambapo vikosi vya Israel vinajiandaa kuanzisha oparesheni ya kulitwaa eneo lote la Gaza. Mpango huo umesababisha ukosoaji mkubwa wa kimataifa, huku viongozi wakionya kuhusu athari mbaya za kibinaadamu katika eneo hilo ambalo tayari limeharibiwa kwa vita.
Huku hayo yakijiri, mashirika ya kigeni yasiyo ya kiserikali yamesema kuwa sheria mpya ya Israel inayodhibiti mashirika ya misaada ya kigeni imekuwa ikitumika zaidi kuwazuia kuingiza misaada Gaza.
Barua ya pamoja iliyosainiwa na zaidi ya mashirika 100 na kuchapishwa Alhamisi, imeeleza kuwa maafisa wa Israel wamekataa maombi yao ya kuingiza misaada ya kuokoa maisha Gaza, wakisema kuwa mashirika hayo hayana mamlaka ya kutoa misaada.
Maombi 60 yakataliwa
Kulingana na barua hiyo, ambayo imesainiwa pia na OXFAM na Madaktari Wasio na Mipaka, MSF, takribani maombi 60 ya kupeleka misaada Gaza ilikataliwa mwezi Julai pekee.
Wakati huo huo, Waziri wa Fedha wa Israel, Bezalel Smotrich mwenye kufuata siasa kali za mrengo wa kulia, ameidhinisha mpango kwa ajili ya ujenzi wa makaazi yanayoitenganisha Jerusalem Mashariki na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu, hatua ambayo ofisi yake imesema itaondoa wazo la kuwepo taifa la Palestina.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ameuzungumzia mpango huo wa kufufua mradi unaojulikana kama E1, ambao Wapalestina na mataifa yenye nguvu duniani wamesema utaugawanya Ukingo wa Magharibi sehemu mbili, na kuna uwezekano ukazusha hasira ya kimataifa.
''Nimetoa maagizo ya kuchapisha mara moja mpango wa kujenga nyumba 3,500 wa E1. Mpango huu ulikuwa umechelewa kwa miaka sita au saba hivi,'' alisisitiza Netanyahu.
Mkutano na wanahabari
Msemaji wa Smotrich amesema kuwa waziri huyo atazungumza na waandishi habari badae leo Alhamisi kuhusu mpango wa ujenzi wa nyumba hizo kwa walowezi wa Israeli katika makaazi yaliyopo Ukingo wa Magharibi na Jerusalem.
Katika hatua nyingine, serikali ya Italia imewapokea Wapalestina 114 walioondolewa Gaza jana usiku, wakiwemo watoto 31 wanaohitaji msaada wa matibabu. Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia, watoto ambao ni wagonjwa wameathirika na majeraha makubwa ama kukatwa viongo vya mwili, au magonjwa waliyozaliwa nayo yenye kuhitaji matibabu maalum.
Aidha, jeshi la Israel limesema Alhamisi kuwa limezuia kombora lililorushwa kutoka Yemen, huku waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran, wamedai kuhusika na shambulizi hilo. Jeshi la Israel limesema kombora hilo limezuiwa na kikosi cha anga.
(AFP, DPA, AP, Reuters)