Wadephul: Ujerumani yajitolea kwa usalama wa Israel
29 Mei 2025Mwanadiplomasia huyo alipoulizwa iwapo Ujerumani inabadili sera yake kuelekea Israel, Wadephul alisema Israel inabakia kuwa mshirika muhimu na wa karibu wa Ujerumani sio tu kwasababu ya historia ya mataifa hayo mawili, akisisitiza kuwa Ujerumani ina jukumu kubwa kwa usalama na uwepo wa taifa hilo la kiyahudi.
Lakini wakati huo huo alitambua kuzorota kwa hali ya kibinaadamu katika ukanda wa Gaza na kuitolea wito Israel kuridhia misaada ya kiutu kufikishwa huko.
Israel yamuua kiongozi mwengine wa Hamas
"Na kile ambacho hakikubaliki ni kwamba, watu katika ukanda wa Gaza hawapati chakula cha kutosha pamoja na dawa. Na hiyo kusema la ukweli ndio jambo ninalozungumza na mwenzangu Gideon Saar, ambaye pia atakuja mjini Berlin hivi karibuni. Israel lazima ijue kwamba tunasimama nao wakati wote, lakini pia tuko pamoja na watu wa Gaza, wao ni binaadamu na kila mtu ana haki ya kupata chakula na dawa, na sisi wajibu wetu ni kuhakikisha hilo linapatikana," alisema Wadephul.
Wadephul yupo mjini Washington Marekani kwa mazungumzo ya kisiasa ambako alikutana na waziri mwenzake wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Marco Rubio.
Ziara yake pia inanuiwa kuweka msingi wa ziara ya Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz mjini Washinton inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni.