Wademocrat wamchagua Ken Martin kuwa mwenyekiti mpya taifa
1 Februari 2025Wanademocrat Jumamosi walimchagua Ken Martin, kiongozi wa chama cha Democrats huko Minnesota, kuwa mwenyekiti wa taifa, wakimgeukia mtendaji wa kisiasa kutoka Midwest mwenye haiba ndogo kuratibu upinzani wao dhidi ya urais wa Donald Trump.
Martin anachukua nafasi ya Jaime Harrison kutoka South Carolina ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Democratic (DNC).
Harrison hakutafuta muhula mwingine baada ya uchaguzi wa 2024 ambapo Trump alikua Mrepublican wa kwanza kushinda kura ya umma katika kipindi cha miongo miwili na kupenya ngome muhimu ya wapigakura wa Democratic - Wamarekani wenye asili ya Afrika, Walatini Amerika na wapigakura wa tabaka la kazi, miongoni mwao.
"Tulipigwa ngumi mdomoni Novemba," alisema Martin, mwenye umri wa miaka 51, Jumamosi. "Ni wakati wa kuinuka, kujikuna na kurudi katika vita hii."
Sasa yeye ni mmoja wa wadau muhimu zaidi katika jaribio la chama cha Democrats kurejea katika mapambano, huku Trump akitanua mipaka ya mamlaka ya urais.
Upigaji kura ulifanyika katika mji wa kitajiri wa Washington ambapo zaidi ya wanachama 400 wa DNC kutoka kila jimbo na eneo la Marekani walikusanyika kwa mkutano wa chama wa msimu wa baridi.
Martin na mgombea mwingine mwenye nguvu, mwenyekiti wa chama cha Democratic huko Wisconsin Ben Wikler, waliahidi kurejesha ujumbe wa Democratic kwa wapigakura wa tabaka la kazi, kuimarisha miundombinu ya Democratic kote nchini na kuboresha mfumo wa haraka wa majibu dhidi ya Trump wa chama cha Democrats.
Waliahidi kutokwepa kujitolea kwa Wanademocrat kwa watu tofauti na makundi ya jamii za wachache, ambyo ni nguzo ya chama cha kisasa. Martin ni mzungu wa kwanza kuongoza DNC tangu 2011.
Soma pia: Barack Obama atarajiwa kuhutubia kwenye siku ya pili ya mkutano wa DNC
Wengine katika kinyang'anyiro walikuwa Martin O'Malley, aliyekuwa gavana wa Maryland na afisa wa utawala wa Biden, na Faiz Shakir, aliyeongoza kampeni ya urais ya Seneta Bernie Sanders kutoka Vermont.
Mgombea Marianne Williamson, mwanaharakati na mwandishi, aliwashangaza wanachama wa DNC kabla ya upigaji kura kuanza kwa kumuidhinisha Martin kama "nafasi yetu bora ya kujitenga na ufisadi unaofadhiliwa na bilionea ambao utazuia na kupunguza uwezekano wetu."
Democrats wakiri changamoto kubwa, bila kuafikiana kilichokwenda vibaya
Wengi wa wagombea walikiri kwamba sifa ya Democratic imeharibiwa vibaya, lakini wachache waliahidi mabadiliko makubwa. Kwa kweli, takriban miezi mitatu baada ya uchaguzi, hakuna makubaliano kuhusu kile kilichokwenda vibaya.
Uchaguzi ulifanyika chini ya wiki mbili baada ya kuapishwa kwa Trump. Wanademocrat wanapambana kukabiliana na mkururo wa amri za rais, misamaha, mabadiliko ya wafanyakazi na uhusiano wenye utata unaochukua sura katika utawala mpya.
Asilimia 31 tu ya wapigakura wana maoni mazuri kuhusu Chama cha Democratic, kulingana na ripoti ya utafiti wa Chuo Kikuu cha Quinnipiac iliyochapishwa wiki hii. Asilimia 43 ya wapigakura wana maoni mazuri kuhusu Chama cha Republican.
Soma pia: Wademokrat wampigia debe Hillary Clinton
Shakir alitoa wito wa kufanyika mabadiliko makubwa ndani ya chama, kama vile ushirikiano zaidi na vyama vya wafanyakazi na kupunguza mkazo kwenye makundi ya wachache kulingana na rangi na jinsia.
Akiwa Muislamu pekee anayewania uenyekiti, Shakir alikuwa peke yake wakati wa kongamano la hivi majuzi la wagombea kupinga kuundwa kwa caucus ya Waislamu katika DNC. Hata hivyo, ugombea wake alishindwa kupata mvuto.
Wikler alikumbana na maswali kuhusu uhusiano wake na mfadhili mkubwa wa Democratic, Reid Hoffman, miongoni mwa waanzilishi wa LinkedIn. Lakini alionyesha kuwa uhusiano wake wa ufadhili ni rasilimali.
Na kimsingi, mwenyekiti wa DNC anatarajiwa kukusanya mamilioni ya dola kuwasaidia Democrats kushinda uchaguzi.