Waathiriwa wa Srebrenica watafuta amani miaka 30 baadaye
11 Julai 2025Zaidi ya Waislamu wa Bosnia 8,000 – wanaume na vijana – waliuawa na vikosi vya Waserbia wa Bosnia baada ya kuuteka mji huo, ambao ulikuwa chini ya ulinzi wa Umoja wa Mataifa.
Mifupa ya Sejdalija Alic na Hasib Omerovic imepatikana na kutambulika rasmi na itazikwa siku ya Ijumaa katika makaburi ya kumbukumbu ya Potocari, wakijumuika na maelfu ya waathiriwa wengine wa mauaji hayo. Hata hivyo, ndugu zao watalaza kaburini mabaki kidogo tu – mfupa mmoja au miwili – wakitumaini kuwa hilo litatosha kuleta amani kwa waliopotea na walio hai.
Mirzeta Karic ambaye amesubiri kwa miongo mitatu, anasema mazishi ya baba yake, Sejdalija Alic, yatakuwa kipindi kigumu zaidi maishani mwake.
"Nimevumilia mengi, lakini mazishi haya ni tukio baya zaidi. Tunazika mfupa mmoja tu. Siwezi kueleza uchungu huu. Ni sehemu ya chini ya taya yake tu iliyopatika. Kuna uwezekano mkubwa, naamini mabaki yake yalipatikana katika makaburi ya pamoja kadhaa. Na wakati miili ilihamishwa kutoka kaburi moja la pamoja kwenda lingine, mifupa yake ilisambaratika."
Sejdalija, maarufu kwa jina la utani “Brko” kwa sababu ya masharubu yake, alikuwa mmoja wa watu wa mwisho kuondoka kijiji cha Jagodnja akiwa na binti yake mnamo Desemba 1993, wakati wa mashambulizi yaliyofanywa na Waserbia wa Bosnia. Wakiwa na mizigo ya kilo 50 ya nafaka na miguu peku wakiwa wamevalia soksi tu, walikimbilia Srebrenica wakitafuta usalama.
Mji wageuka kuwa mtego wa mauti
Srebrenica ulikuwa umetangazwa na Umoja wa Mataifa kuwa “eneo salama,” lakini badala yake ni mji uliogeuka kuwa mtego wa mauti kwa makumi ya maelfu ya raia wa Bosnia waislamu waliokuwa wamekimbilia humo.
Baadaye, Karic aliondolewa Srebrenica kupitia msafara wa Msalaba Mwekundu pamoja na mama yake na shemeji yake mjamzito, huku baba yake na kaka yake wakibaki nyuma. Hakuwahi kuwaona tena. Miaka kadhaa baadaye, kaka yake Sejdin, aliyeuawa akiwa na umri wa miaka 22, alizikwa mwaka 2003.
Miaka 30 tangu mauaji ya kikatili ya Srebrenica, bado karibu waathiriwa 1,000 hawajapatikana. Maelfu ya miili ya waliouawa ilihamishwa kwa kutumia mitambo mizito na kutupwa katika makaburi ya siri, kwa lengo la kuficha uhalifu uliotokea. Mifupa mingi iliharibika vibaya, na kuacha wataalamu wa uchunguzi wa vinasaba wakifanya kazi ya kuunganisha vipande vilivyopatikana ili kuwatambua wahanga.
Mfupa wa taya ndio uliopatikana wa Alic – sawa na Hasib Omerovic, ambaye naye atazikwa Ijumaa. Hasib alikuwa na umri wa miaka 33 alipochukuliwa pamoja na kaka yake, na inaaminika waliuawa katika moja ya maeneo makuu matano ya mauaji ya halaiki ya Srebrenica. Familia yao ilitengana Julai 11, 1995.
Kwa familia nyingi za waathiriwa wa Srebrenica, kama za Karic na Omerovic, amani bado ni ndoto ya mchana – lakini angalau kuzika hata mfupa mmoja kunatoa nafasi ya mwisho ya heshima na nafasi ya kuomboleza.