Waasi wadaiwa kutenda ukatili mkubwa Mashariki mwa Kongo
20 Agosti 2025Ukatili huo ni pamoja na kuwabaka wanawake kwa makundi, kuwaua raia kiholela na kushambulia hospitali katika eneo la mashariki mwa Kongo.
Katika ripoti yake mpya iliyopewa jina "DRC: ‘Walisema tungekufa': Ukiukaji wa M23 na Wazalendo Mashariki mwa Congo”, Amnesty inasema waasi wa M23 wameua raia bila kufuata sheria, kuwateka wagonjwa na kuwatesa wanaharakati wa kiraia. Wakati huo huo, makundi ya Wazalendo yamekuwa yakipewa silaha na risasi kwa wingi na jeshi la Congo, hali inayochochea uhalisia wa kivita eneo hilo. Mkurugenzi wa Amnesty kwa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini Tigere Chagutah, amesema ukatili wa pande hauna mipaka.
Qatar: Kongo na M23 bado wamo kwenye mchakato wa amani
Amnesty International iliwahoji zaidi ya watu 53, wakiwemo waathirika wa ubakaji wa makundi, ndugu wa waliouawa, madaktari, wanaharakati, wanasheria na waandishi wa habari. Ripoti hiyo ilikamilishwa pia kwa kutumia ushahidi wa picha, video na taarifa za mashirika ya haki za binadamu ya ndani na kimataifa.
Ushuhuda wa wanawake kutoka Kivu Kaskazini na Kivu Kusini unaonesha kiwango cha ukatili huo. Wanawake 14 waliosimulia walibakwa kwa makundi. Beatrice kutoka Bukavu alisema alivamiwa na wanajeshi watano wa M23.
"Kwa wanawake wa mashariki mwa DRC, hakuna mahali salama; wanabakwa majumbani mwao, mashambani au hata kambini wanakokimbilia,” alisema Tigere Chagutah, akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kusisitiza ulinzi wa raia hasa wanawake na watoto wanaobeba mzigo mkubwa wa vita hivi.
Mbali na ubakaji, M23 pia imenyanyasa wanaharakati, waandishi wa habari na wanasheria. Wengine waliteswa, kutoweshwa kwa nguvu au kushikiliwa bila sababu. Shirika hilo lilithibitisha pia visa vya mauaji ya raia, wakiwemo wanaume watatu mjini Goma na baba na mwanawe huko Kivu Kusini, waliouawa kati ya Februari na Mei 2025.
Mapigano yazuka tena mashariki mwa Kongo
Amnesty International ilisema mashambulizi ya M23 yalijumuisha hata hospitali, ambako wagonjwa na wahudumu walitekwa au kushikiliwa. Haya yalitokea kati ya Februari na Mei mwaka huu, wakati kundi hilo lilikuwa likidhibiti sehemu kubwa ya Goma na Bukavu.
Wakati Congo na M23 wakisaini "tamko la kanuni” mjini Doha tarehe 19 Julai, na kukubaliana kuendeleza mchakato wa amani ulioanzishwa Washington mwezi Juni, Amnesty imetoa wito kwa Qatar na Marekani kuwataka wahusika wote kusitisha ukatili, kusimamia uwajibikaji na kuhakikisha hakuna mpiganaji anayehusishwa na ukiukwaji mkubwa wa haki anayeendelea kushiriki katika mchakato wa amani.