Waasi wa M23 wasema watabakia Goma
31 Januari 2025Corneille Nangaa ameyasema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari jana Alhamisi na kuongeza kuwa watasalia Goma, hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa M23 kutoa taarifa kwa umma tangu wapiganaji wake walipouvamia mji huo unaokaliwa na mamilioni ya watu siku ya Jumatatu.
Kwenye mkutano huo aidha, Nangaa alitangaza kile alichokiita "maandamano ya ukombozi" kuelekea mji mkuu, Kinshasa, wakilenga kuiangusha serikali ya Rais Felix Tshisekedi.
Soma pia: UN yatiwa wasiwasi na ripoti za M23 kusonga mbele Bukavu
Lakini Tshisekedi mwenyewe alisema hawatakubali kuangushwa na waasi na kutoa wito kwa umma wa eneo la mashariki kuwazuia wapiganaji hao wanaojaribu kuchukua maeneo zaidi.
Waziri wa Ulinzi wa Kongo, Guy Kabombo, amesikika kupitia ukanda wa video akisema kwamba ameagiza kufutwa mara moja mipango yote ya mazungumzo na waasi hao na kusema watabakia Kongo kupambana kufa na kupona.